Migne: tutakazia stars Kasarani

Tuesday July 30 2019

 

By Thomas Matiko

BAADA ya kutoka sare tasa na Taifa Stars juzi Jumapili mjini Dar es Salaam kwenye mchuano wa kufuzu kushiriki dimba la CHAN 2020, Kocha wa Harambee Stars, Mfaransa Sebastian Migne kawataka vijana wake kukaza buti timu hizo zitakaporudiana Jumapili.

Kulingana na Migne, vijana wake walionyesha unyonge sana katika kipindi cha kwanza ila baada ya mapumziko mafupi ndipo walifufuka.
“Kipindi cha kwanza hatukucheza vizuri, tulijivuta sana ila nafikiri katika kipindi cha pili tulikuwa afadhali kidogo. Bado tuna fursa ya kufuzu tutakaporudiana nao wikendi nyumbani. Tutastahili kucheza vizuri zaidi ya tulivyofanya kule kwao” Migne kasema. Taifa Stars walikuwa wanasaka kulipiza kisasi ya kulimwa na Harambee mabao 3-2 kwenye dimba la AFCON kule Misri wiki chache zilizopita ila kwa mara nyingine wakafeli.  
Ili kufuzu kwa raundi ya pili, Stars wanahitaji ushindi wa aina yoyote kwani sare ya mabao itawatupa nje kutokana na kuwa hawakuweza kupata bao la ugenini.
Timu itakayoibuka bingwa baada ya mechi ya marudiano wikendi itakayochezewa Uwanja wa Kasarani, atakutana na Sudan. Mshindi wa mechi hiyo dhidi ya Sudan ambayo pia itapigwa ugenini na nyumbani atajikatia tiketi ya moja kwa moja ya kujiunga na hatua ya makundi ya dimba hilo la CHAN 2020 ambalo huhusisha tu wachezaji wa ndani.
Taifa Stars walishindwa kuifungua difensi ya Harambeee Stars licha ya mabadiliko makubwa yaliyofanyika katika kikosi hicho na hasa ikizingatiwa wenyeji hao walikuwa na wachezaji wanane kikosini mwao, waliounda timu ya kule Misri.
Hata ahadi ya Dola 5,000 (Sh519,200) kutoka kwa serikali ya Tanzania bado haikutosha kuwapa motisha Taifa Stars  kuwazidi Harambee ambao wamekuwa wakiwahangaisha kwa muda.

Advertisement