Miezi 10 ya Morrison Tanzania

MIKIKIMIKIKI anayopitia winga wa Simba, Benard Morrison tangu atue kucheza soka la Tanzania, ndio sababu ya jina lake kutokauka midomo mwa mashabiki wa Simba na Yanga.

Kutokana na hilo, uongozi wa Simba umeshauriwa kumkalisha chini na kumjenga ili aweze kuendana na tamaduni za Tanzania, licha ya Afrika Kusini alikotokea kuonekana staili ya maisha yake kuwa ya kawaida.

Mwanaspoti limekuchambulia maisha ya Morrison tangu ajiunge na Yanga, Januari mwaka huu, usajili wake, walichosema wadau na wana saikolojia.

MIEZI SITA YANGA

Morrison alijiunga na Yanga, Januari mwaka huu kwa mkataba wa miezi sita, akiwa mchezaji huru, ameacha alama ya kuifunga Simba mechi ya mzunguko wa pili ya msimu ulioisha.

Mashabiki wa Yanga ilikuwa ikifika, Machi 8 walikuwa wanaiita Morrison Day, huku shabiki maarufu Frank Yanga katika gari yake aliandika jina la mchezaji huyo na kubandika picha yake kama kuumiza wafuasi wa Simba.

Kipaji cha mchezaji huyo, jinsi alivyokuwa na umalidadi wakutembea juu ya mpira, pasi za visigino na aina yake ya ushangiliaji wa kunyanyua mguu mmoja juu, huku akitembelea na mikono, ulibamba sana akiwa Yanga na ulipa kicheko mashabiki wa timu hiyo.

Ukiachana na hilo, Morrison aliwahi kukiri kwa jinsi ambavyo mashabiki wa Yanga walivyoonyesha ukarimu baada ya kuifunga Simba, umemshangaza.

USAJILI WAKE SIMBA

Kitendo cha uongozi wa Simba kutangaza kummiliki Morrison kilizua tafrani kwa wadau wa soka na uongozi wa Yanga uliamua kwenda kushitaki katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ambako kesi yake iliwachukua muda kuiamua.

Mashabiki wa Simba, Yanga walikuwa wanakwenda kupiga kambi nje ya ofisi za TFF, zilizopo Karume jijini Dar es Salaam, huku usalama wao ukilindwa na polisi, baada ya kuamliwa atakuwa mali ya Simba, Yanga ilikata rufaa kwenda CAS.

Ukiachana na hilo, uongozi wa Yanga uliibua jipya tena baada ya kutangaza mkataba wa Morrison, haukuwa na saini ya Simba, jambo hilo likapelekwa tena TFF.

MAISHA YAKE SIMBA

Wakati wa utambulisho wake rasmi, Agosti 22 mwaka huu, Morrison alipewa nafasi ya kuongea na alikiri anaipenda Simba, huku akifanya vituko vya hapa na pale vilivyogeuka shangwe kwa mashabiki wa timu hiyo, waliokuwa wakimzomea akiwa Yanga.

Ukiachana na mikimiki ya hapa na pale ya Morrison, ikiwemo usajili wake ulichukua muda mrefu, tayari amefungiwa kucheza mechi tatu, kutokana na kosa la kumpiga ngumi beki wa Ruvu Shooting, Juma Nyoso, wakati wa mchezo wao, ulipigwa Uhuru, Simba ikipoteza kwa bao 1-0.

Kutokana na matukio hayo, Morrison amekuwa akitazamwa kwa mitazamwa kwa mitazamo tofauti na mashabiki wa Simba ambao baadhi wanamkingia kifua, huku wa Yanga wakichukizwa na tukio hilo.

AONJA JOTO

Morrison ameonja joto la jiwe kwa mashabiki wa klabu kongwe, akiwa Yanga walikuwa wanamshangilia kama mfalme, baada ya kuwahama wanamwona kaishiwa kiwango, wakimponda na amebakia jina.

Simba nao wanamwona kama mfalme baada ya kuwa mchezaji wao, tofauti na alivyokuwa Yanga na walikuwa hawakubali kiwango chake, wakimponda kazi yake nikupanda mipira lakini hana maajabu yoyote.

WADAU WATOA NENO

Beki wa zamani wa Simba na Yanga, Godwin Aswile alisema tukio la Morrison liliwahi kumkumba mwaka 1992 kutoka Jangwani kwenda Msimbazi, anafichua kilichomsaidia kuwa ni utulivu.

“Kiukweli kelele za mashabiki wa Simba na Yanga zina nafasi kubwa ya kumuathiri mchezaji, anachotakiwa Morrison ni kukaa na sababu zinazotafutwa kwake, acheze kwa nidhamu, pia asikamie kwamba ngoja niwaonyeshe uwezo mashabiki wa Simba atashindwa, bali awe mvumilivu kila kitu kitakaa sawa,” alisema Aswile na aliongeza kuwa,

“Kama Simba hawatamtafutia Morrison mwana saikolojia, hawezi kumaliza ligi kwani kelele zimezidi kwake, mimi nilikalishwa chini baada ya kutoka Yanga kwenda Simba ndio maana nilifanikiwa, wamsaidie ili atimize majukumu yake kwa amani,” alisema.

Naye straika wa zamani wa Simba na Yanga, Thomas Kipese alisema Morrison aachane na habari za mashabiki afanye kazi yake kwa utulivu, akiamini ndicho kitu kitakachomsaidia kuonyesha kiwango chake.

“Awe mtulivu na asipanie kufanya vitu, kama Simba imemsajili waliona uwezo wake, kwani kuna kipindi mchezaji anaweza akawa anapitia changamoto ambazo zinatakiwa zitatuliwe na utulivu na sio vurugu,” alisema.

APATA MTETEZI

Mwana saikolojia, Charles Nduki alisema ikitokea wanachama, mashabiki na viongozi wakatengeneza chuki kwa Morrison ni rahisi kupunguza ufanisi wake wa kazi, akiwa uwanjani, anachoshauri ni kupata mtu wa kumjenga, kujua ni jinsi gani ya kuzimudu changamoto hizo.

“Morrison ana kipaji kikubwa kama ilivyo kwa Mario Balotel, shida yao ni moja ya nidhamu mbovu, ambayo inaweza ikasababishwa na jamii, malezi na mazingira aliyokulia, ndio maana inakuwa ngumu kuwalaumu moja kwa moja, kinachotakiwa ni viongozi wa timu wanazochezea kuwajenga kiakili ili kuendana na utamaduni wao,” alisema Nduku na aliongeza kuwa,

“Afrika Kusini alikotokea Morrison, maisha anayoishi kule niyakawaida, ingawa kwetu tunaona ni ya ajabu, kinachoweza kumuathiri ni kule kuzomewa, akili ya binadamu ili ifanye kazi kwa ufasaha inatakiwa isiingiliwe na jambo lolote,” alisema.