Michuano ya njiwa usipime

Muktasari:

Hapo awali sikuelewa siri ya nyimbo za taarabu kumjumuisha njiwa wala kufahamu mapenzi ya watu wengi kwa ndege huyu au kupelekea sehemu nyingi za mjini na hasa Mji Mkongwe kuwepo maeneo ya wazi ya watu kuwapelekea njiwa chakula asubuhi na

Kila nikijaribu kusahau na kuona ni mambo ya zamani niliyokutana nayo wakati nikienda shule nafsi huniambia haiwezekani kusahau kwa sababu ni sehemu ya maisha yangu.

Ni hadithi ndefu inayojirudia na kunikumbusha nilipokuwa mdogo. Nayo ni njiwa aliyezungumziwa kwa njia tofauti kila siku asubuhi katika nyimbo za taarabu za Zanzibar wakati nakwenda shule.

Miongoni mwa nyimbo zilizosikika kila siku katika sauti ya Unguja inao ubeti usemao “Njiwa peleka salamu kwa wangu muhibu, fika ukamwambie kwake ninapata tabu.” Nilipovuta umri nilielewa kuwa njiwa ana visa na mikasa katika ulimwengu wa mahaba ya watu wa Zanzibar.

Hapo awali sikuelewa siri ya nyimbo za taarabu kumjumuisha njiwa wala kufahamu mapenzi ya watu wengi kwa ndege huyu au kupelekea sehemu nyingi za mjini na hasa Mji Mkongwe kuwepo maeneo ya wazi ya watu kuwapelekea njiwa chakula asubuhi na jioni.

Nakumbuka alikuwepo mzee mmoja wa Kihindi ambaye jioni alifika Forodhani na kuwamwagiwa njiwa mtama na kuwapatia juisi kwenye vifuu. Hivi karibuni nilipoangalia runinga nilikumbuka zama zangu za utotoni niliposikia simulizi za mashindano ya kuruka na urembo wa njiwa.

Mashindano ya huyo ndege wa mahaba hufanyika katika nchi nyingi za Ulaya, Marekani, Amerika Kusini, Canada, nchi za Asia na Afrika Kusini. Hawa njiwa hushindana kuruka masafa tofauti kati ya kilomita 100 (maili 62) na hadi kilomita 1,000 (maili 620). Lakini Marekani imeweka rekodi ya kuwa na mashindano ya kilomita 1,800 (maili 1,100).

Michuano ya njiwa huwa ni kali na mshindi hutangulia kumaliza kwa kumpita aliyekuwa nyuma yake kwa sekunde chache. Historia inaonyesha mchezo huu ulianzia Ubelgiji mwaka 1830 kwa mashindano ya kilomita 160 (maili 100) kutoka Paris, Ufaransa hadi Liege, Ubelgiji na baadaye kutoka London hadi Ubelgiji 1823.

Njiwa wanaoshiriki mashindano wanaenziwa kwa kupatiwa huduma muhimu kama chakula kizuri, matibabu na malazi ya raha. Njiwa hawa ni waliotimiza umri wa miezi sita na wasizidi umri wa miaka mitatu. Muda wanaoshi njiwa wengi ni kati ya miaka mitatu hadi mitano, lakini wachache hufikisha hadi 15.

Kasi yao ya kuruka inafikia kilomita 130 (maili 81) kwa saa wanaposukumwa na upepo na hali ikiwa shuwari ni ya wastani wa kilomita 80 (maili 50). Hawa njiwa hupewa mafunzo ya kuepuka kugongwa na ndege angani, kuepuka kugongana na ndege wenzao wanapokuwa wanashindana, kuepuka giza ya mawingu au katika hali yoyote ya hewa ili wapae juu zaidi.

Vyama na vilabu vya mbio za njiwa vimeunda shirikisho la kimataifa na vina gazeti linalotoa habari za njiwa na mashindano ya kitaifa na kimataifa.

Katika baadhi ya nchi kama Brazil, mashindano makubwa ya mbio za njiwa huandaliwa na serikali huku katika baadhi ya nchi na hasa India, China, Pakistan, Iran, Ufilipino, Japan, Taiwan na Bangladesh mbio hizo huwa na msisimko mkubwa kwa watu wa rika zote.

Taiwan inaongoza kwa kuwa na mashindano mengi ya njiwa duniani na inakisiwa karibu njiwa nusu milioni hushiriki na zawadi zinazotolewa kwa washindi huwa kibunda cha mamilioni ya fedha, magari na vitu vingine vya thamani.

Mashindano makubwa ya kimataifa ni pamoja na ya Olimpiki na mara ya mwisho yalifanyika katika mji wa Poznan, Ubelgiji mwezi Januari, mwaka jana.

Katika mashindano yaliyofanyika Afrika Kusini yaitwayo The Million Dollar Pigeon Race (Mashindano ya Njiwa ya Dola Milioni Moja) yalishirikisha njiwa 4,300 waliotoka nchi 25 na zawadi ziliaotolewa zilikuwa na thamani ya Dola 1.3 milioni za Kimarekani.

Utakapoelezwa bei ya njiwa wanaosifika kwa kushinda mashindano ndio utapigwa na butaa.

Kwa mfano, tajiri mmoja wa China alimnunua njiwa aitwaye Armando aliyekuwa anamilikiwa na Mholanzi kwa Dola 328,000 za Kimaekani na baadaye aliuzwa kwenye mnada kupitia katika mtandao kwa mfanyabiashara wa China kwa Euro 1.25 milioni. Huyu Armando anajulikana kama Flying Messi (yaani Messi anayeruka) kumfananisha na mchezaji kandanda maarufu wa Argentina, Lionel Messi. Lakini wakati Lionel anatamba ardhini huyu Armando hashikiki angani.

Njiwa huyu ameshinda mbio za kimataifa za Uholanzi, Ulaya na Olimpiki na kubeba medali za dhahabu na zawadi za fedha.

Kabla ya hapo njiwa walionunuliwa kwa pesa nyingi na matajiri wa China ni Bolt (Dola 310,000 katika mwaka 2013), Nadine (Dola 400,000 mwaka 2017) na New Bliksem (Dola 376,000 mwaka 2018).

Kilichojitokeza karibuni ni baadhi ya wamiliki kuwapa njiwa dawa za kuwaongezea nguvu.

Hatua hiyo imesababisha njiwa kupimwa kama hawatumii hizo dawa kabla ya mashindano.

Mwaka jana, Romania ilitayarisha mashindano ya mbio za nyika yaliyoshirikisha karibu njiwa 20,000 na hii ni rekodi ya dunia ya wengi kushiriki katika mashindano.

Siku hizi zipo nchi ambazo zikifanya mashindano ya mbio (riadha) pia huwa na mashindano ya kutafuta njiwa mrembo.

Katika mashindano ya kutafuta njiwa mrembo yaliyofanyika Irak Februari 22, mwaka jana njiwa 300 wa kike na kiume walishiriki.

Kwa kweli haya sio madogo. Kuishi kwingi kuona mengi, hata katika medani ya michezo.