Miamba hii 11hatarini TPL

Thursday May 16 2019

 

By Thobias Sebastian

LIGI Kuu Bara imefikia patamu. Kwa sasa ipo ukingoni na mwishoni mwa mwezi huu itafikia tamati na kufahamika bingwa wa msimu huu wa 2018-2019.

Kuhitimishwa kwa ligi hiyo na kupatikana bingwa kuna maana Tanzania itakuwa imeshapata mwakilishi rasmi wa Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu ujao wa 2019-2020, lakini pia timu tatu zitakazoshuka daraja kwenda Ligi Daraja la Kwanza (FDL), ingawa African Lyon imetangulia mapema na kuacha nafasi mbili za wazi kwa klabu nyingine.

Ukiondoa Simba iliyokonafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi iliyobakiwa na michezo mitano kabla ya msimu kumalizika timu nyingine zote zimebaki na michezo isiyozidi miwili mpaka mitatu.

Kutokana na msimamo wa ligi ulivyo timu nane tu ndio zina nafasi ya kubaki msimu ujao, huku nyingine 11 zilizosalia zipo kwenye hatihati kutokana na tofauti ya pointi zilizopo sasa na idadi ya mechi zilizosalia kabla msimu haujafungwa.

Timu nane ambazo zipo salama katika msimamo na zimejihakikishia nafasi ya kuwepo msimu ujao ni vinara Yanga inayoongoza msimamo ikiwa na alama 83 kutokana na mechi 36, watetezi Simba walio nafasi ya pili na pointi zao 82 ikicheza mechi 33 na Azam inayokamata nafasi ya tatu na alama zake 69 baada ya mechi 36.

Nyingine ni KMC, Mtibwa Sugar kila moja ikiwa na alama 49, kisha kufuatiwa na Lipuli yenye pointi 48, Ndanda yenye alama 47 na Singida United yenye pointi 45.

Kati ya hizo nane ni Yanga na Simba ndizo zipo kwenye mbio za ubingwa, huku Azam ikijihakikisha kumaliza nafasi ya tatu na nyingine zitabadilishana nafasi kulingana na jinsi zitakavyocheza mechi zao zilizosalia.

HIZI KAZI ZINAZO 

Ukiachana na timu hizo nane ambazo zipo katika mahala salama kuna nyingine 11, ambazo mbali ya kubakiwa na michezo isiyozidi mitatu hazipo mahali salama kama zitashindwa kufanya vizuri michezo yao iliyobaki kwa maana ya kupata ushindi zaidi ya kupoteza.

Katika msimamo kuanzia timu iliyokuwa nafasi ya tisa Coastal Union yenye pointi 44, haipo mahali salama kwani Mwadui iliyokuwa nafasi ya 19, ikiwa na pointi 38, kama itashinda mechi zake mbili za mwisho itafikia pointi ambazo Coastal kama itashindwa kupata ushindi katika mechi tatu alizobaki nazo.

Timu 11, ambazo hazipo mahala salama na pointi zao kwenye mabano ni Coastal iliyokuwaa nafasi ya tisa, Mbao (44), Mbeya City (43), Tanzania Prisons (43), Kagera Sugar (43), Ruvu Shooting (42), Alliance (41), Stand United (41), JKT Tanzania (41), Biashara United (40), na Mwadui (38).

Kama timu hizo zitachemsha na zitajikuta zikiangukia kwenye nafasi ya 17 na 18 zijue mapema kuanza playoff dhidi ya timu za Ligi Daraja la Kwanza zinazochuana kwa sasa zinawahusu ili kuwania nafasi ya kushuka ama kubaki kwenye Ligi Kuu msimu ujao.

MSIKIE DK LEAKEY

Mchambuzi wa masuala ya soka nchini, Dk. Leakey Abdallah alisema hali ilivyo kwenye ligi kwa sasa inaonyesha namna baadhi ya timu huwa kama zipozipo tu ndani ya ligi hiyo.

“Inaonesha kiasi gani kuna timu ambazo viwango vyao ni vidogo na huenda zikawa sehemu ya kuchangia kushuka kwa ushindani katika ambao kama ungekuwepo tungekuwa na timu nyingi ambazo zina uhakika wa kuwepo msimu ujao na chache ndio zingekuwa hazina uhakika lakini hilo limekuwa kinyume chake,” alisema.

Advertisement