Mhini aula England kusoma, kujifunza kuogelea klabu ya St Felix

Muktasari:

Muogeleaji wa chipukizi wa Tanzania, Dennis Mhini aliyeiwakilisha nchi katika mashindano ya vijana ya Olimpiki yaliyofanyika nchini Argentina na kuhimarisha muda wake katika staili ya backstroke na freestyle kwa mita 50 na 100. Matokeo yake mazuri katika kuogelea na darasani yameifanya shule na klabu maarufu ya mchezo wa kuogelea nchini England kumpa nafasi ya kusoma na kujifunza mchezo huo.

Dar es Salaam. Muogeleaji wa klabu ya Morogoro (Mis Piranha), Dennis Mhini anatarajia kuondoka nchini Ijumaa kuelekea Uingereza tayari kujiunga na klabu na shule maarufu ya St Felix anayotamba kwa mchezo wa kuogelea nchini humo.

Dennis aliiwakilisha Tanzania katika michuano ya vijana ya Olimpiki iliyofanyika mjini Buenos Aires, Argentina amepata nafasi hiyo baada ya kukidhi vigezo viwili.

Kigezo cha kwanza ni ubora wake katika mchezo kuogelea baada ya kufikia muda unaotakiwa na pili uwezo wake wa darasani.

Akizungumza jijini baba wa mchezaji huyo, Hamis Mhini alisema mwanaye pamoja na kutoweza kutwaa medali Argentina, alifanikiwa kupunguza muda wake wa kuogelea, jambo ambalo limewavutia walimu na kocha maarufu wa mchezo wa kuogelea nchini Uingereza, Sue Purchase.

Mhini alisema kuwa wazazi na ndugu wengine wamefarajika sana kuona ndugu yao anajiunga St Felix na kuahidi kumsaidia kwa ari na mali.

Katika michezo ya Olimpiki ya Vijana, Dennis alimaliza nafasi ya tatu katika kundi la kwanza kweye staili ya freestyle ya mita 100 kwa kupata muda wa sekunde, 58.53 na pointi 514 na vile vile kumaliza katika nafasi ya tatu kwa upande staili ya backstroke kwa mita 50 kwa kutumia sekunde 29.79 na kupata pointi 525.

 “Siyo kuogelea tu, wenzetu wapo makini sana kwa upande wa masomo pia. Amefikia viwango walivyoweka na kumpatia nafasi ambayo nasi tunagharimia baadhi ya mahitaji, ni fursa kwa muogeleaji nan chi pia,” alisema Mhini.

Kwa upande wake, Dennis alisema kuwa amefarijika sana kupata nafasi hiyo na kuwahsukuru wazazi na chama cha kuogelea kwa ushirikiano mkubwa.

“Nimepata uzoefu mkubwa sana kwenye michezo ya Olimpiki ya vijana, Buenos Aires, Argentina, mashindano yalikuwa magumu na kufanikiwa kuweka muda mpya, nafasi ya kujiunga na St Felix imekuwa kipindi muafaka, nitajitahidi nihimarishe muda wangu na kufuzu katika mashindano ya Olimpiki, Jumuiya ya Madola nay a dunia,” alisema Dennis.

Dennis alisema kuwa atakuwa anapata mafunzo, lishe na vifaa bora mbali ya makocha ambao wana uwezo mkubwa.