Mhilu awapiga mkwara Dube na Kagere

Mshambuliaji Yusuph Mhilu wa Kagera Sugar amesema licha ya kuwaona washambuliaji wenzake Meddie Kagere wa Simba na Prince Dube wa Azam FC wakitupia katika msimu huu, jambo hilo halimtishi kwani naye bado ana nafasi ya kufanya kitu.

Akizungumza na Mwananchi, Mhilu alisema kitu pekee ambacho kilimchelewesha katika ligi msimu huu ni baada ya kuumia nyama za paja mwanzoni mwa msimu.

“Msimu huu nina malengo ya kufunga magoli 20, hili kwa upande wangu naona kabisa kwamba naweza kufanya hivyo nikiendelea kupata nafasi kwa sababu hata hao wanaofunga timu nyingine inatokana na kupata muda wa kucheza mara kwa mara,” alisema Mhilu.

Akizungumzia hali yake ya kiafya, alisema ameanza kukomaa polepole tofauti na maumivu ambayo aliyokuwa nayo alipoumia wakati akijiandaa na mchezo dhidi ya JKT Tanzania.

“Nashukuru Mungu naendelea vizuri japokuwa sio sana, lakini sina maumivu kama ambavyo ilikuwa siku ya kwanza, naamini nitakuwa katika ubora zaidi,” alisema.

Mshambuliaji huyo mpaka sasa ameshaifungia Kagera Sugar mabao mawili katika mechi mbili ikiwa ni dhidi ya KMC waliyoshinda 1-0 na Azam FC ambapo timu yake ilipoteza kwa mabao 4-2.

Katika msimu uliopita mshambuliaji huyo aliifungia Kagera Sugar mabao 13 na kuwa katika orodha ya wafungaji bora wa msimu huo, lakini hakuwa na papara ya kuondoka na kuamua kuongeza mkataba wa miaka miwili kuwa na klabu hiyo.