Mhilu afichua kilichomfanya aitose Yanga

Muktasari:

Mhilu, beki David Luhende na kocha wao Mecky Maxime walikuwa wakihusishwa na mipango ya kutua Jangwani kuungana na Zawadi Mauya aliyetangulia mapema

YUSUF Mhilu kalelewa na kukuzwa Jangwani na hivi karibuni mabosi wake wa zamani walikuwa wakimpigia hesabu kumrejesha kikosini, lakini ghafla jamaa kabadilisha gia hewani na kusaini mkataba wa miaka miwili na kuanika sababu kilichomzuia asirejee Yanga.

Mhilu, beki David Luhende na kocha wao Mecky Maxime walikuwa wakihusishwa na mipango ya kutua Jangwani kuungana na Zawadi Mauya aliyetangulia mapema, lakini wote kila mmoja amesaini mkataba wa miaka miwili katika klabu hiyo ya mjini Bukoba na straika huyo chipukizi amefunguka.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mhilu aliyemaliza ligi iliyopita akiwa na mabao 13 alisema kilichomfanya aipotezee ofa ya Yanga ni mustakabali wa mdogo wake, Dickson Mhilu ambaye alihakikishiwa na mabosi wake kama atasaini mkataba mpya watamchukua ili acheze naye Kagera.

Yaani ule msemo wa damu nzito kuliko maji ama udugu kufaana ndio alioutumia Mhilu aliyetua Kagera akitokea Ndanda aliyoichezea kwa mkopo baada ya Yanga kumuachia msimu uliopita na mwenyewe alisema ameamua kubaki Kagera kwa sababu ya mdogo wake tu. Mhilu mdogo alikuwa anacheza Simba U20 katika ushambuliaji na Kagera ilipotaka kumuongezea mkataba alitoa sharti kuwa lazima mdogo wake huyo asajiliwa Kagera ili asalie la sivyo anasepa zake.

Inaelezwa sharti hilo halikuwa tatizo kwa mabosi wa klabu hiyo na kuamua kumpa fasta mkataba wa miaka miwili na kumtekelezea jambo lake, ilimradi tu asiwakimbie na kwenda Yanga, wakati bado wanahitaji huduma yake.

Mhilu alipotafutwa na Mwanaspoti ili kufafanua juu ya taarifa hizo za kutoa sharti la kusajiliwa kwa mdogo alikiri ni kweli amesajili miaka miwili Kagera sambamba na mdogo wake, ila akadokeza kuna kipengele cha kumruhusu kuondoka muda wowote akipata timu nje ya nchi.

“Ndio nimeshasaini nimeona bora nibaki hapa hapa kwa sababu ya mdogo wangu ambaye wamemsajili, nimesaini miaka miwili ila uzuri mkataba hautanibana kama nitapata timu ya nje, kwa hapa ndani haitakuwa rahisi kuondoka na kama watanitaka ni lazima waonane na mabosi wangu Kagera,” alisema.

Pia alidokeza isingekuwa rahisi kwake kutimkia Yanga kwa ofa aliyowekewa mezani na uongozi wa klabu yake ulioonyesha nia ya dhati ya kumbakisha na yeye akiwa ameipa kipaumbele, kadhalika kusajiliwa kwa mdogo wake na kumpa mshahara mzuri, hakuona sababu ya kuondoka klabuni hapo.