Mhilu: Tatizo ni mabeki wanakamia

STAIKA Yusufu Mhilu anayeichezea klabu ya Kagera Sugar amesema katika mechi zilizosalia amekuwa akikamiwa na mabeki wa timu pinzani kiasi cha kuzidi kupata wakati mgumu anapokuwa yupo uwanjani.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mhilu alisema anatambua kwamba mabeki wanamkamia kutokana na kuwa miongoni mwa wafungaji wenye magoli mengi lakini na yeye anaendelea kupambana nao.

“Kuna wakati mgumu naupata katika kipindi hiki kiukweli, kila timu tunayokutana nayo mabeki wake wananikamia kweli lakini sijakata tamaa bado,” alisema.

Mhilu alitolea mfano mchezo wao waliopoteza dhidi ya Polisi Tanzania kwamba mabeki wapinzani walimkamia lakini muamuzi alikuwa kama haoni.

“Hata goli tulilopata katika mchezo huo ilitokana na mimi kufanyiwa madhambi nje ya boksi lao tukapata faulo iliyozaa goli, lakini katika kipindi cha pili ilikuwa hatari,” alisema.

Mhilu anashika nafasi ya pili katika ufungaji akiwa na magoli 13 huku nafasi ya kwanza ikishikiliwa na Meddie Kagere mwenye mabao 20 (kabla ya mechi ya jana Simba dhidi ya Alliance).