Mhasibu wa TFF aangua kilio Mahakamani kesi yao kupigwa kalenda

Muktasari:

  • Aliyekuwa Mhasibu wa (TFF) Nsiande Mwanga na aliyekuwa Rais wa (TFF) Jamal na Katibu wa TFF, Mwesigwa Selestine wakikabiliwa na mashitaka 28, ikiwemo ya utakatishaji fedha ambazo ni Dola za Marekani, 375,418.

Dar es Salaam. Aliyekuwa Mhasibu wa (TFF) Nsiande Mwanga ameangua kilio baada ya upande wa mashtaka kuieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa mashahidi walioandaliwa kwa ajili ya kutoa ushahidi wamepata udhuru kesi haitoweza kuendelea.

Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Leonard Swai amedai mahakamani hapo kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kusikiliza, lakini mashahidi walioandaliwa leo wamepata udhuru

"Siku ya leo hatuna mashahidi wiki iliyopita niliwapa taarifa, lakini wana udhuru mmoja amefiwa na mwingine amesafiri naiomba mahakama ipange tarehe nyingine.

Baada ya maelezo hayo Hakimu Hakimu, Maila Kasonde aliutaka upande wa mashtaka kuhakikisha shauri hilo linapokuja mahakamani wanakuwepo mashahidi walioandaliwa.

Hakimu Kasonde aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 30, 2019 kwa ajili ya kusikilizwa.

Washtakiwa wengine ni aliyekuwa Rais wa (TFF) Jamal na Katibu wa TFF, Mwesigwa Selestine ambao wakikabiliwa na mashitaka 28, ikiwemo ya utakatishaji fedha ambazo ni Dola za Marekani, 375,418.

Miongoni mwa mashtaka hayo ni inadaiwa, Malinzi na Selestine walighushi nyaraka ya maazimio ya kamati tendaji kwa lengo la kuonesha kuwa kamati hiyo ya TFF imelenga kubadili mtia saini wa shirikisho hilo katika akaunti za benki kutoka Edgar Masoud kwenda kwa Mwanga.