Mguu nje vyuma vitano kung’oka Old Trafford

MADRID, HISPANIA. IKIWA dirisha kubwa la usajili majira ya joto linatarajiwa kufungwa Oktoba 5, bado kuna wachezaji ambao muda wowote huenda wakakamilisha usajili wa kutoka kwenye klabu zao za sasa kwenda timu nyingine ambazo zinatamani huduma zao.

Miongoni mwa wachezaji hao ni wale wa Manchester United ambao baadhi yao wamekuwa hawana nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza kwa sababu kocha Ole Gunnar Solskjaer haonekani kuwa na mpango wa kuwatumia msimu huu. Mwanaspoti linakuletea orodha ya wachezaji watano ambao huenda wakaondoka Man United dirisha hili.

Andreas Pereira

Msimu uliopita alishika namba tatu kwa kuwa mchezaji wa tatu kutengeneza nafasi nyingi za kuzalisha mabao ambazo ni 30, nyuma ya Fred aliyeshika nafasi ya kwanza kwa kutengeneza 35, na Marcus Rashford akishika nafasi ya pili kwa kutengeneza nafasi 32. Staa huyu a anatajwa kuwa na nafasi kubwa ya kuondoka.

Katika dirisha hili la usajili, klabu za PSG na Lazio ni miongoni mwa timu zinazoimezea mate saini yake ingawa Lazio imeonekana kuwa mbele zaidi kwenye harakati hizo.

Jesse Lingard

Lingard ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwakani amekuwa sio sehemu ya kikosi cha kwanza cha Man United kwa muda mrefu baada ya kiwango chake kushuka. Hali hiyo imeifanya timu kufikiria kumuuza na klabu nyingi zimeonekana kuhitaji saini yake, ikiwa ni pamoja na Everton na Inter Milan. Lingard kwa sasa ana umri wa miaka 27. amecheza mechi 208 na kufunga mabao 33, tangu apandishwe kikosi cha kwanza mwaka 2011.

Juan Mata

Alijiunga Man United mwaka 2014 na mpaka sasa amecheza mechi 180 akifunga mabao 33.

Lakini kwa muda misimu miwili sasa ameonekana kuwa hana kiwango kizuri ingawa amepata nafasi kubwa ya kucheza. Msimu uliopita mwezi Januari alicheza dakika 205, Febuari akacheza 88, Machi dakika 18, Juni tisa na Julai alimaliza kwa kucheza dakika kumi. Ujio wa Bruno Fernandes unaonekana kufifisha matumaini yake ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha Kocha Solskjaer.

Phil Jones

Beki huyu msimu uliopita alicheza mechi nane na kufunga bao moja. Amekuwa sio chaguo la kwanza la Kocha Solskjaer huku vijana Axel Tuanzebe na Timothy Fosu-Mensah wanaonekana kuchukua nafasi yake. Jones huenda akawafuata wachezaji wenzake kina Ashley Young aliyetua Inter Milan na Chris Smalling anayewindwa vikali na AS Roma. Kwa sasa amepata majeraha ya goti ambayo yanazidisha uvumi kwamba hawezi kusalia tena Old Trafford.

Chris smalling

Staa huyu ana asilimia chache sana za kusalia Man United kwa sababu Roma inapambana kuhakikisha inamsainisha mkataba wa moja kwa moja, baada ya kuonyesha kiwango bora msimu uliopita alipojiunga nayo kwa mkopo wa msimu mmoja. Mkataba wake Man United unatarajiwa kumalizika mwaka 2022, Solskjaer haonekani kuwa na mpango wa kutaka kumtumia katika kikosi chake kwa msimu huu. Inter Milan pia inaimezea mate saini yake.