Mgunda: Bocco amekosa uungwana kwa Singida United

Muktasari:

Simba illibuka na ushindi wa mabao 2-0 katika mchezo huo na kutawazwa kuwa bingwa mpya wa Ligi Kuu msimu huu akitetea taji hilo huku akiwa na michezo miwili mkononi.

Dar es Salaam. Wakati mjadara wa bao la nahodha wa Simba, John Bocco ukiendelea, kocha mkuu wa Coastal Union, Juma Mgunda amesema kitendo cha Bocco kufunga bao hilo kumemkosesha heshima ya fair play.

Bocco aliiandikia Simba bao la pili katika mechi iliyowapa ubingwa dhidi ya Sindida United jana kwenye uwanja wa Namfua mkoani Singida.

Nahodha huyo wa Simba alifunga bao huku kipa wa Singida, Said Lubawa akiwa chini ameumia baada ya kupiga mpira kuokoa ili usiwe kona, aliumia na kubaki chini nje ya uwanja akiomba msaada.

Hata hivyo mechi haikusimama na Bocco kuandika bao kipa akiwa nje ya uwanja ambapo baada ya kuumia hakuweza kuendelea na mchezo na nafasi yake kuchukuliwa na Robert David.

"Hakuna sheria ya fair play ni uungwana tu, hivyo ilikuwa ni Bocco kuonyesha uungwana," amesema Mgunda.

Amesema kama nahodha huyo wa Simba angeonyesha uungwana kwenye mchezo huo, Leo hii angepata heshima kubwa tofauti na bao alilofunga.

"Labda hakumuona, lakini hata mchezaji wa Simba aliyerusha mpira, alipaswa kuanza kuonyesha uungwa, lakini kama walitumia advantage ya kuumia kwa kipa wa Singida kupata bao, basi hawakuonyesha uungwana," alisema Mgunda.