Mgunda : Kikapu kilinipa mke kama utani!

Muktasari:

Mwanaspoti limefanya mahojiano na nyota huyo wa zamani ambapo amefunguka mambo mbalimbali.

“MPIRA wa kikapu unashindwa kuendelea kutokana na mfumo wa uendeshaji kubadilika, tofauti na miaka ya nyuma ulipokuwa ukipewa kipaumbele shuleni na vyuoni,” anasema nyota wa zamani wa mpira wa kikapu nchini, Bahati Mgunda na kuongeza kuwa, ndio uliowakutanisha na mwanamke aliyemuoa.

Mgunda anazungumzia mambo mengi kuhusu mchezo huo na faida alizopata, wakati akicheza na hata baada ya kustaafu kucheza, lakini akiendelea na majukumu ya uongozi ikiwemo kuibua vipaji kwa vijana.

Mwanaspoti limefanya mahojiano na nyota huyo wa zamani ambapo amefunguka mambo mbalimbali.

NAFASI YA SERIKALI

Anasema mchezo huu unaweza kurudisha hadhi ikiwa serikali na wadau wa mchezo huo watawekeza, pia hata kuwapa motisha wachezaji wenye mapenzi na mchezo huo.

“Mfumo wa kuendesha mashindano haya kwa kuupeleka mchezo huu kwenye mashindano ya shule za msingi (Umitashumta) na sekondari (Umisseta), inaweza kusaidia kurudisha hadhi yake na kuibuka vipaji vingi vya vijana,” anasema.

“Tanzania imejaaliwa vipaji, shida ni kuviibua kuanzia chini kwa kuwapa uzoefu vijana wakiwa shuleni na baadaye kijiunga na klabu za majeshi ikiwa ni sambamba na za watu binafsi ili kupata ajira,” anasema.

MFUMO MBOVU

“Miaka yetu wachezaji tulikuwa wachache na tulikuwa tunafanya vizuri kutokana na kuandaliwa mazingira ya kujifunza tukiwa katika ngazi za shule, lakini sasa ni mapenzi ya mchezaji mwenyewe kujitafutia mwalimu wa kumfundisha,” anasema.

Anasema mfumo wa ukuzaji vipaji vya wachezaji ni mbovu jambo ambalo amewashauri viongozi wa juu kulifanyia kazi kwa kuurudisha mchezo huo shuleni na vyuoni.

“Shule nyingi zipo jirani, hivyo walimu wanaweza kuanzisha ligi za shule ama vyuo kwa mchezo huo ili kuzalisha vipaji vingi zaidi,” anasema.

MAJESHI YAPEWA KIFYAGIO

“Tofauti kubwa iliyopo ni timu za majeshi kupewa kipaumbele sana na kusikika zaidi kutokana na wachezaji wake kuwa ndani ya ajira, lakini kipindi cha nyuma timu zote zilikuwa na umaarufu na zilikuwa zikipewa kipaumbele kutokana na uwezo,” anasema.

“Timu za majeshi zimejizolea umaarufu kwa kutoa ajira nyingi kwa vijana wenye uwezo wa kucheza mchezo huu kuanzia mtaani kutokana na uwezo wao uwanjani,” anasema.

Anasema kwa miaka ya hivi karibuni timu za mpira wa kikapu zimeongezeka zaidi baada ya udhamini wa Kilimanjaro kuutangaza zaidi mchezo huo na kuwawezesha vijana kujifunza na kujikita katika huu mchezo.

WADHAMINI NI ISHU

Soka ndio linalopewa kipaumbele Tanzania kutokana na wadhamini wengi kuwekeza huko na kusahau kabisa michezo mingine ambayo pia imekuwa ikifanya vizuri ndani na nje.

Anasema mchezo wa mpira wa kikapu unaonekana kutofanya vizuri kutokana na kukosa chachu ya ushindani kutoka kwa timu na timu kutokana na kukosa udhamini ambao ungechangia kuinua ari wachezaji kujituma zaidi.

“Huu mchezo haujashuka, bado unafanya vizuri ngazi zote, lakini timu kushindwa kuonesha ushindani kama zamani ni ukosefu wa wadhamini ambao ndiyo chachu ya kuinua vipaji kwa wachezaji,” anasema.

NAMNA YA KUKUZA VIPAJI

“Nawashauri viongozi kuwa na mfumo endelevu wa kuwasaidia vijana ili wawe na morali ya kucheza mpira wa kikapu na kutafuta wadhamini ambao watatoa zawadi kwa wachezaji ili waweze kucheza kwa kushindana,” anaeleza namna ya kukuza vipaji.

“Pia, uongozi unatakiwa kujaribu kuandaa mfumo ambao utasaidia kuwa na mashindano ya mara kwa mara ili kuwajengea uwezo wachezaji ambao wamekuwa wakijifunza mchezo huo, wakiwa na umri mkubwa tofauti na wale wanaoanza wakiwa na umri mdogo,” anasema.

UTANDAWAZI UNAZOROTESHA KIKAPU

Wakati Watanzania wengine wakinufaika kutokana na matumizi ya mitandao ya kijamii ikiwa ni sambamba na utandawazi ambao umekuwa maarufu sana kwa sasa basi unaambiwa kwa upande wa kikapu imekuwa ni changamoto.

Hayo yamebainishwa na Mgunda akiweka wazi kuwa imekuwa ikiwanyima fursa wachezaji wa mchezo huo kuamini katika kufundishwa na kujikuta wakitumia YouTube au CD kujifunza zaidi kitu ambacho kimekuwa sababu ya kuuangusha mchezo huo.

“Zamani wachezaji tulikuwa tunafundishwa, lakini kwasasa wengi wanajifunza kupitia mikanda ya video na CD, pia wapo wanaojifunza kupitia kwa kushuhudia mapambano yanayoonyeshwa kwenye televisheni.

“Kuna wachezaji wengi wanaotakiwa kufuatwa kutokana na uchezaji wao, lakini changamoto kubwa ni namna ya kujifunza, hivyo ni vigumu kupata wachezaji wazuri wa kuwapa changamoto wachezaji chipukizi,” anasema Mgunda.

“Napenda sana safari. Hivyo, naweza kusema kikapu kimetimiza ndoto yangu kwani nimefanikiwa kusafiri sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi. Pia mchezo wa kikapu umenipa ajira ya ualimu wa mchezo huo inayoniwezesha kuendesha maisha yangu,” anasema.

CHANGAMOTO NI MOJA TU

Wakati Watanzania waliowengi wakishindwa kufikia malengo yao kutokana na kukatishwa tamaa na changamoto wanazokutana nazo kwenye majukumu wanayofanya, Mgunda amewatoa hofu na kuwataka kuendelea kupambana zaidi kwani changamoto ni moja ya njia ya mafanikio.

“Nawashauri waendelee kujifunza, pamoja na changamoto wanazozipata, wanatakiwa kutambua kuwa, kikapu ndiyo ajira yao hapo baadaye hivyo, wanatakiwa kupambana na kuwasikiliza vizuri walimu wao kila wanapopata nafasi ya kujifunza,” anasema.

MGUU ULIMWEKA NJE

Bahati anabainisha kuwa anajivunia kuwa miongoni mwa wacheza kikapu wa miaka hiyo japo kuna muda alitamani kuachana na mchezo huo.

“Ni mengi sana niliyokumbana nayo, lakini kubwa ni lile lililonisababisha kushindwa kucheza michuano mbalimbali katika muda wa mwaka mmoja baada ya kuvunjika mguu,” anasema.

“Tukio jingine nikiwa kama kocha, nilitukanwa na mchezaji wa timu pinzani mbele ya wachezaji wangu, tukio hili nilitamani niachane na mpira wa kikapu lakini watu wangu wa karibu ikiwa ni sambamba na wachezaji wangu waliniambia nichukue kama changamoto,” anasema.

AMUANGUKIA MAGUFULI

Bahati anaamini wajibu wa kodi wanaokumbana nao wafanyabiashara umechangia anguko la mchezo huo kutokana na wawekezaji kushindwa kuidhamini ligi hiyo.

“Nikipata nafasi ya kuonana na Rais John Magufuli ningemwomba aweze kutoa punguzo la kodi kwa kampuni zinazojitokeza kwa lengo la kuwekeza katika michezo,” anasema.

“Unajua kuna kampuni nyingi zinatamani kuingiza bidhaa zao za michezo nchini kwa lengo la kuwekeza, lakini zinashindwa kufanya hivyo kutokana na kukwepa kodi,” anasema.

“Mbali na hilo, nikipata nafasi hiyo nitamwomba rais arudishe mashindano shuleni ili viibuliwe vipaji kuanzia ngazi ya shule za misingi, sekondari hadi vyuo vikuu.”

ALIVYOPATA MKE

“Najivunia vitu vingi sana kupitia mchezo huu na ndiyo ulionipatia mke. Nilimpata katika mashindano ya kikapu. Najivunia hicho pia umenifanya nionane na watu wengi na kusafiri katika nchi nyingi,” anasema Bahati ambaye alikuwa anacheza timu ya Vijana.

“Tulikutana katika mashindano kwenye viwanja vya Don Bosco na nilimpenda kutokana na ubora wake kwenye mchezo huo naye pia alikuwa ni mcheza kikapu, haikuwa kazi ngumu kwangu kwani nilikuwa namvizia mazoezini na kwenye mashindano,” anasema Bahati ambaye amebainisha kuwa hakuwahi kushiriki mashindano yoyote kwenye kikosi cha timu ya taifa ya mpira wa kikapu kutokana na timu kutokuwa na mashindano hadi alipostaafu.