Mgeveke atoa neno kwa mastaa wa Yanga

Muktasari:

Beki wa Mwadui FC, Joram Mgeveke ametoa ushuhuda wa namna safu ya ushambuliaji ya Yanga ilivyo moto, baada ya kucheza nao jana Ijumaa ya Oktoba 9, mwaka 2020.

BEKI wa Mwadui, Joram Mgeveke amezungumzia mechi yao ya kirafiki na Yanga, kwamba imewapa picha ya namna gani wanatakiwa kujipanga, kuhakikisha wanakuwa wanapata matokeo mazuri kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.

Katika mechi hiyo, iliyopigwa jana Ijumaa ya Oktoba 9, mwaka 2020, Mgeveke alikuwa mwiba wa kutibua kazi nzuri ya washambuliaji wa Yanga, ambapo alikuwa anaondosha mashambulizi langoni kwao ili wasifungwe.

Mgeveke amekiri Yanga ina kikosi kizuri chenye wachezaji wenye uzoefu, hivyo mechi hiyo, anaamini imewapima na kuwaweka kwenye mstari sahihi.

"Yanga wamesajili vizuri msimu huu, ingawa kikosi chao bado kinaonekana bado hawajazoeana vya kutosha, ila naamini kadri muda utakavyokuwa unakwenda watakaa vizuri na watakuwa na ushindani mzuri,"amesema Mgeveke na ameongeza kuwa.

"Kwa upande wa kikosi chetu nakiamini kipo vizuri ingawa kina vijana wengi, wapambanaji ndio maana tumeonyesha ushindani wa hali ya juu kwenye mechi hiyo, licha ya kwamba Yanga wakatumia vyema nafasi dakika za mwishoni wakafunga,"amesema.
 
Katika msimamo wa ligi kuu Bara, Mwadui ipo nafasi ya nane, katika mechi tano walizocheza wameshinda mbili, wamefungwa  tatu, hivyo wamejikusanyia pointi sita.