Mgawo wa mkwanja kwa kila timu EPL msimu uliomalizika

Muktasari:

  • Hivi ndivyo mgawo wa pesa ulivyotoka kwenye timu za Ligi Kuu England msimu huu.

LONDON,ENGLAND.MANCHESTER City imetetea ubingwa wao wa Ligi Kuu England kibabe baada ya vuta nikuvute kwenye mbio za kuusaka ubingwa huo dhidi ya Liverpool.

Man City iliichapa Brighton 4-1 kwenye mechi ya mwisho ya msimu na Liverpool wao waliichapa 2-0 Wolves na hivyo kumaliza vita hiyo ya ubingwa, ambapo mshindi akipatikana kwa tofauti ya pointi moja, 98 kwa 97.

Bingwa, timu zilizoshika Top Four zimepatikana na hata zilizoshuka daraja pia zimeshafahamika. Kwenye ligi hiyo kuna mgawo wa pesa, ambapo timu ya juu kwenye msimamo, inakuwa inapokea nyongeza ya kama Pauni 2 milioni tofauti na ile ya chini yake, hivyo hadi inayoshika mkia kwenye ligi.

Timu zilizoshuka daraja, zitapata kiasi kidogo cha pesa, lakini itaendelea kupokea pesa kwa misimu minne ijayo ili kuwasaidia kurudi tena kwenye Ligi Kuu England.

Hivi ndivyo mgawo wa pesa ulivyotoka kwenye timu za Ligi Kuu England msimu huu.

Huddersfield Town kwa kushika nafasi ya mwisho kwenye msimamo, yenyewe imelipwa Pauni 1.9 milioni, wakati Fulham ya juu yake imepata Pauni 3.8 milioni, huku Cardiff City walioshika daraja pia, lakini wao wameshika nafasi ya 18, wamepata mgawo wa pesa Pauni 5.8 milioni.

Kwenye nafasi ya 17, Brighton wamepata Pauni 7.7 milioni, wakati Southampton waliokuwa nafasi ya juu yao wamepata Pauni 9.6 milioni na Burnley kwenye nafasi ya 15 imepata mgawo wa Pauni 11.5 milioni.

Bournemouth wao wamepata mgawo wa Pauni 13.4 milioni, wakati Newcastle United waliopo juu wamevuna Pauni 15.4 milioni na Crystal Palace wamepata Pauni 17.3 milioni, huku Watford kwenye nafasi ya 11 wamevuna Pauni 19.2 milioni na West Ham United waliokamatia nafasi ya 10, wamekusanya mkwanja wa Pauni 21.1 milioni.

Kwenye nafasi ya juu, Leicester City, wamevuna Pauni 23.1 milioni, wakati Everton kwenye nafasi ya nane wameweka kibindoni Pauni 25 milioni na Wolves nafasi ya saba imewafanya wavune Pauni 26.9 milioni.

Manchester United watakaocheza Europa League msimu ujao kwa kushika nafasi ya sita kwenye ligi, wao wamepata mgawo wa Pauni 28.8 milioni, wakati Arsenal kwenye nafasi ya tano imevuna Pauni 30.7 milioni na ndani ya Top Four, wakianza Tottenham katika nafasi ya nne, wamevuna Pauni 32.6 milioni, Chelsea kwenye nafasi ya tatu, Pauni 34.6 milioni na Liverpool nafasi ya pili wamekamatia Pauni 36.5 milioni, wakati Manchester City namba moja na mabingwa, wamepata mgawo wa Pauni 38.4 milioni ikiwa ni mgawo wa Ligi Kuu England.