Mfumo mpya Klabu Bingwa Ulaya huu hapa...

Muktasari:

Baada ya janga la corona, mechi za kumalizia michuano ya Ulaya zitafanyika kuanzia Agosti

Zurich, Uswisi. Msimu wa soka wa 2019/20 barani Ulaya utamalizwa kwa wiki tatu za mchakamchaka wa kila siku wakati watakaposakwa mabingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya na Europa League.

Baada ya janga la corona, mechi za kumalizia michuano ya Ulaya zitafanyika kuanzia mwezi ujao.

Ligi za ndani zimepewa nafasi ya kumalizika mwishoni mwa mwezi huu, huku Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa), likipanga kumalizia mechi mwezi ujao ili kwenda na kasi ya kuanza kwa msimu wa 2020/2021.

Mabadiliko mengine kwenye michuano hiyo ni kwamba hakutakuwa na mechi za nyumbani na ugenini, badala yake itakuwa mechi moja na timu ikichapwa inatolewa huku michezo hiyo ikipigwa kwenye viwanja huru bila mashabiki. Ligi ya Mabingwa Ulaya itafanyika Ureno kwenye viwanja vya Estadio da Luz na Estadio Jose Alvalade, wakati ile ya Europa League itapigwa Ujerumani kwenye viwanja vya Cologne, Duisburg, Dusseldorf na Gelsenkirchen.

Mikikimikiki hiyo itaanza kwa mechi za Europa League hatua ya 16 bora, ambapo zitapigwa Agosti 5 na Agosti 6. Agosti 21 inatarajiwa kuchezwa fainali ya Europa League uwanjani RheinEnergieStadion, Cologne, huku siku mbili baadaye itapigwa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya uwanjani Estadio da Luz.