Messi vs Ronaldo : Messi apitia kipindi kigumu

Muktasari:

Ni wachezaji bora, wanaopendwa zaidi, wanaofuatiliwa zaidi, wanaovutia wengi, kwa kuangalia juu juu unaweza kudhani kuwa ni jambo ambalo lipo sawa, kila kitu kinakwenda vizuri lakini nao wana kupanda na kushuka kama ilivyo kwa mwingine yeyote.

TOLEO lililopita, Mwandishi, Luca Caioli alielezea namna ambavyo Ronaldo alikuwa na furaha baada ya kutwaa taji la Ulaya ‘Euro 2016’ akiwa na Timu ya Taifa ya Ureno na kueleza kuwa hayo ndiyo mafanikio aliyokuwa akiyawaza kwa muda mrefu. Sasa endelea…

“Hiki ni kitu ambacho nimekuwa nikikitaka tangu mwaka 2004, hiki ndicho kinachoifaa Ureno, nchi inatakiwa kupata hiki, wakati wote nimekuwa nikiamini kuwa hawa wachezaji wana ujasiri, uwezo na mbinu kutoka kwa kocha wetu za kuifunga Ufaransa na tumeweza.

“Hii ni hatua ambayo haiwezi kusahaulika,” alisema Ronaldo akifahamu kuwa taji hilo ni kitu ambacho wachezaji wachache wameweza kufanikisha kulipata.

Ni wachezaji bora, wanaopendwa zaidi, wanaofuatiliwa zaidi, wanaovutia wengi, kwa kuangalia juu juu unaweza kudhani kuwa ni jambo ambalo lipo sawa, kila kitu kinakwenda vizuri lakini nao wana kupanda na kushuka kama ilivyo kwa mwingine yeyote.

Yafuatayo ni baadhi ya matukio yenye changamoto katika maisha ya soka ya Ronaldo na Messi.

Kuanzia fainali za Kombe la Dunia za Brazil mwaka 2014, katika ndoto zake zote mbaya, Messi hakuwahi kuwaza fainali ya aina hii.

Katika dakika karibu zote 120, Messi alikuwa akielekea katika kuitimiza ndoto yake ya kuwa bingwa wa dunia na Timu ya Taifa ya Argentina lakini wakati dunia yote ikijiaminisha mechi kuelekea kwenye hatua ya mikwaju ya penalti, bao la kimaajabu la Mario Gotze lilimshusha Messi na kuwa pigo kubwa kwake. Ujerumani, mahasimu wa muda mrefu wa Argentina walifanya kweli kwa mara nyingine na pengine wanafahamu vyema namna ya kuzifuta ndoto zao. Walifanya hivyo katika namna ya kusikitisha katika hatua ya robo fainali Afrika Kusini mwaka 2010 na walifanya hivyo pia mwaka 2006 katika ardhi yao ya nyumbani kwenye mikwaju ya penalti.

Mara ya mwisho kwa timu hizo kukutana katika fainali nyingine ilikuwa ni mwaka 1990 pale Italia, Wajerumani katika tukio hilo walipambana hadi hatua ya mwisho na hatimaye kulibeba taji katika penalti ya utata iliyojazwa wavuni na Andreas Brehme katika dakika ya 86.

Ilikuwa ni kama kujibu mapigo kwa kile walichokumbana nacho miaka minne iliyopita kule Mexico katika fainali nyingine za Kombe la Dunia, Argentina ilibeba taji lake la pili la dunia na mpinzani wao kwenye fainali hakuwa mwingine bali ni Ujerumani.

Hiyo ilikuwa fainali ya Diego Armando Maradona, ni kama ambavyo fainali za mwaka 2014 zilivyokuwa zikitajwa kwamba ni fainali za Messi.

Messi alibeba matumaini na ndoto za timu yake ya Taifa mabegani, akiwa na matumaini ya kuipa mafanikio nchi yake kama ilivyokuwa mwaka 1978 na 1986, alikuwa na dhamira moja, kuiongoza timu yake kwenye mafanikio kama alivyofanya Maradona enzi zake, wote ni wachezaji wawili bora katika historia ya soka la Argentina.

Hata Maradona mwenyewe alimtaja Messi kuwa ndiye mrithi wake lakini wanaotofautishwa kwa kipindi cha miaka 30 pamoja na tofuati kubwa kwenye bahati. Brazil haikuwa kama ambavyo Messi alitaka, kwa mtu ambaye huwa anashinda mara kwa mara kushika nafasi ya pili ni kushindwa kunakoumiza. Katika mechi hiyo ya fainali iliyopigwa Juni 13, 2014, Messi alicheza mchezo usio wa kawaida, haukutosha kukumbusha anapokuwa na Barcelona, matukio kadhaa ya maana lakini hakuwa na maajabu kwa sana. Baada ya kuanza vizuri fainali za Brazil, Messi aliishia kurudi nyumbani mikono mitupu, kweli alitwaa tuzo ya kiatu cha dhahabu akiwa mchezaji aliyeng’ara katika mashindano hayo lakini pamoja na uzuri wake lakini ilikuwa kama haina maana.

Zaidi ya hilo kukawa na mijadala yenye utata kuhusu Messi kama alitakiwa hata kupewa tuzo hiyo, baadhi ya watu akiwamo Maradona mwenyewe alisema kwamba timu ya watu 13 walioteuliwa na Fifa kufanya uamuzi huo waliangalia umaarufu na si ubora.

Itaendelea Jumanne ijayo…