Messi sasa anamtaka Mane atue Barcelona

Muktasari:

Mane amekuwa kwenye kiwango bora kabisa huko kwenye kikosi cha Liverpool kwa sasa akiwasaidia kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England na kutinga hatua ya robo fainali kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

BARCELONA, HISPANIA . LIVERPOOL mmesikia hii? Ni hivi, si unajua huko Barcelona, straika Luis Suarez ameshaanza kuchoka kwa maana ya umri kumtupa mkono.

Si unajua staa huyo moto mkali kwenye kufunga mabao alitua Barcelona akitokea Liverpool? Basi bana supastaa wa maana huko Nou Camp, ambaye akisema lake lazima lifanyiwe mchakato, Lionel Messi amewaambia viongozi wa Barcelona, kwamba anamtaka Sadio Mane kwenye kikosi hicho.

Messi ndiye nahodha wa Barcelona na amewaambia mabosi kwamba Mane ndiye mchezaji anayetaka asajiliwe kwenye dirisha lijalo la usajili wa majira ya kiangazi huko Ulaya.

Mane amekuwa kwenye kiwango bora kabisa huko kwenye kikosi cha Liverpool kwa sasa akiwasaidia kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England na kutinga hatua ya robo fainali kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Fowadi huyo Msenegali amekuwa moto, akifunga mabao 20 msimu huu, huku mabao yake 11 akiyafunga katika mechi 11 za karibuni alizocheza kwenye michuano yote.

Mane alicheza mara mbili wakati Liverpool walipoisukuma nje Bayern Munich kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na kiwango chake kilimvutia Messi na kumtaka aje Barcelona.

Barcelona imekuwa na kawaida kwenda kubeba mastaa huko Liverpool ambapo ukimweka kando Suarez, Januari mwaka jana ilikwenda kumnasa kiungo Philippe Coutinho. Bodi ya Barcelona inaamini Mane wakimnasa watakuwa wamempata Samuel Eto’o mpya kwenye kikosi chao ili kuongeza makali na mapambano ya michuano.