Messi aweka rekodi ambazo hazivunjiki

Muktasari:

Messi aliweka reodi ya kufunga mara nyingi mfululizo kwenye mechi za ligi. Staa huyo alifunga mabao 33 katika mechi 21 mfululizo kwenye La Liga msimu wa 2012/13.

BARCELONA, HISPANIA
NANI anabisha kwamba Lionel Messi ni mchezaji anayelifahamu goli pengine kuliko kitu kingine chochote kile anapokuwa ndani ya uwanja.
Staa huyo wa Kiargentina kwa huduma yake hiyo bora kabisa katika kufunga mabao imeipa faida kubwa Barcelona, lakini jambo jingine ni kumsaidia katika kuweka jina lake juu kabisa katika vitabu vya rekodi kwa sababu amekuwa akivunja kama anavyopenda.
Cheki hapa mabao ya Messi yalivyomfanya kuweka rekodi kibao kwenye soka ambazo hakika hutarajii kuona zikivunjwa katika kipindi cha miaka ya karibuni. Hizi rekodi ni ngumu kuvunjwa.

5.Kufunga mfululizo kwenye mechi za ligi
Ndio maana wanasema unapokuwa na huduma ya Lionel Messi kwenye kikosi chako, basi unakuwa umeshajihakikishia kushangilia mabao kutokana na uhodari wa mchezaji huyo.
Messi aliweka reodi ya kufunga mara nyingi mfululizo kwenye mechi za ligi. Staa huyo alifunga mabao 33 katika mechi 21 mfululizo kwenye La Liga msimu wa 2012/13.

Katika msimu huo, Messi aliifunga kila timu iliyokuwa kwenye ligi na hivyo kuweka rekodi matata kabisa.
Hii ni rekodi ambayo Messi ilimfanya avunje ile ya gwiji wa Bayern Munich, Gerd Muller, ambaye alikuwa amefunga mabao 22 katika mechi 16 mfululizo za ligi msimu wa 1969/70.

4.Mabao mengi kwenye klabu moja
Rekodi hii inahusisha Ligi Kuu tano bora kabisa za Ulaya. Messi amekuwa kwenye kikosi cha Barcelona tangu utoto wake na hajahama kwenye timu hiyo. Kiwango chake cha kufunga kimemfanya kuwa mchezaji anayeongoza kwa mabao mengi kuifungia timu moja kuliko mchezaji mwingine yeyote kwenye Ligi Kuu tano bora za Ulaya kwa maara ya La Liga, Bundesliga, Serie A, Ligue 1 na Ligi Kuu England, hakuna mchezaji mwingine aliyefunga mabao mengi kwenye timu moja kumzidi Messi.
Staa huyo amefunga mabao 573 katika mechi 657 na kuweka rekodi hiyo ya kufunnga mara nyingi kwenye timu moja katika klabu hizo za Ulaya.
Hii ni rekodi ambayo Messi aliivunja kutoka kwa Gerd Muller, ambaye alikuwa akishikilia baada ya kufunga mabao 525 kwenye mechi 574 alizochezea Bayern Munich.

3.Mabao mengi ndani ya mwaka mmoja
Suala la kufunga mabao halijawahi kuwa gumu kabisa katika maisha yake ya kisoka. Kufunga na kufikisha mabao 50 ndani ya msimu ni kitu ambacho Messi amekuwa akikifanya mara nyingi sana.
Mwaka 2012 staa huyo wa Nou Camp aliweka rekodi kwa kufunga mabao mengi ndani ya mwaka huo, wakati alipoweka kwenye nyavu mipira mara 91 katika mechi za klabu yake ya
Barcelona na Timu ya Taifa ya Argentina.
Hayo ndio mabao kwa jumla wake kwenye mechi zote alizocheza kwa mwaka huo. Messi alifunga mabao 79 kwenye mechi 60 alizoichezea Barcelona kwa mwaka huo, wakati kwenye kikosi cha Argentina alifunga mabao 12 katika mechi tisa na hivyo kuwa na wastani mzuri kabisa wa mechi na bao. Hii ni rekodi itakayosubiri kwa miaka mingi sana kuvunjwa, yaani atokee mchezaji atakayefunga mabao yanayoanzia 92 ndani ya mwaka mmoja.

2.Mabao mengi kwenye La Liga
Messi ndiye kinara wa kihistoria wa mabao kwenye La Liga baada ya kuweka wavuni mipira mara 398 katika mechi 433. Idadi hiyo ya mabao ni zaidi ya 87, aliyomzidi mchezaji anayeshika namba mbili kwa kufunga mara nyingi kwenye historia ya La Liga, ambaye ni Cristiano Ronaldo. Lakini, Ronaldo kwa sasa ameshahama kwenye ligi hiyo na kutimkia huko Italia kwenye Serie A, jambo litakalomfanya pengo la mabao kuwa kubwa zaidi kwa sababu Messi yeye bado anakipiga kwenye kikosi cha Barcelona. Kwa sasa
mchezaji mwenye mabao mengi anayefuatia ambaye bado yupo kwenye La Liga ni Aritz Aduriz wa Athletic Bilbao, aliyefunga mabao 154 katika mechi 399. Kwa sasa Aduriz ana
miaka 31, hivyo hawezi kuvunja rekodi hiyo.

1.Mchezaji mdogo kushinda Ballon d’Or mara nne
Supastaa Messi ameshinda Tuzo ya Ballon d’Or mara tano na alikuwa mchezaji mwenye umri mdogo kushinda tuzo hiyo katika awamu zake nne za mwanzo. Muargentina huyo
alibeba tuzo nne akiwa na umri wa miaka 25 tu.
Kitu kingine, Messi aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kwenye historia ya Tuzo ya Ballon d’Or baada ya kunyakua kwa miaka minne mfululizo. Rekodi ya kubeba Ballon d’Or kabla ya kufikisha miaka 25 itadumu kwa muda mrefu na inaweza kuchukua muda kuona rekodi hiyo ikivunjwa ukiweka kando ile ya kubeba tuzo hiyo mara nne
mfululizo.