Messi awapandisha presha Inter Milan

Tuesday November 6 2018

 

Milan, Italia. Nyota wa Barcelona, Lionel Messi huenda akawepo kwenye kikosi cha timu hiyo ambacho kinatarajiwa kuivaa Inter Milan kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya leo Jumanne usiku licha kuripotiwa kuwa majeruhi wiki mbili zilizopita.

Hata hivyo nyota hiyo wa Argentina ameshangazwa  jina lake kutajwa kuwa katika orodha ya kikosi cha wachezaji ambao wamesafiri kuifuata Inter Milan.

Messi aliumia wiki tatu zilizopita wakati timu yake ilipokuwa kwenye mchezo wa La Liga dhidi ya Sevilla ambao iliibuka na ushindi wa mabao 4-2.

Messi alikosa mechi ya El Clasico dhidi ya Real Madrid, ambapo Barca iligawa kipigo cha mabao 5-1, pia alikosa mechi ambayo kikosi hicho kiliiadhibu Inter Milan mabao 2-0.

Messi amerejea kwenye mazoezi na wachezaji wenzake wiki iliyopita lakini ilitarajiwa kwamba angekuwa nje ya uwanja kwa wiki nyingine zaidi.

Kocha wa Barcelona, Ernesto Valverde  alisema hakutangaza kuwa Messi asicheza bali kutokana na hali yake walimpumzisha ili aweze kurejea kwenye hali yake haraka.

Barcelona inaongoza kwenye Kundi B baada ya kushinda mechi zake zote za Ligi ya Mabingwa Ulaya wakati wapinzani wao Inter Milan wamejikita nafasi ya pili ambapo kwa namna yoyote wanatafuta ushindi kwenye mchezo wa leo dhidi ya wababe hao wa soka wa Hispania.

Advertisement