Messi atisha pesa ndefu duniani

Muktasari:

  • Messi ameingiza kiasi cha Pauni 100 milioni kwa mwaka huku akimtoa katika kiti hicho bondia maarufu wa Marekani, Floyd Mayweather ambaye alishika nafasi hiyo kwa miaka minne kati ya miaka saba iliyopita.

LONDON,ENGLAND . NDANI na nje ya uwanja Lionel Messi ni mbabe. Safari hii siyo kwa wanasoka tu, bali kwa wanamichezo wote. Ameongoza katika orodha ya wanamichezo wanaolipwa zaidi duniani kwa mwaka huu wa fedha.

Messi pia amempiku hasimu wake wake mkuu, Cristiano Ronaldo aliyeshika nafasi ya pili chini yake pamoja na staa wa kimataifa wa Brazil, Neymar aliyeshika nafasi ya tatu na hivyo kufanya nafasi zote tatu za juu kushikwa na wanasoka.

Orodha hiyo inajumuisha mishahara, bonasi na pesa za matangazo ya biashara kwa wanamichezo kuanzia Juni Mosi 2018 hadi Juni Mosi 2019 na Messi anakoga noti kuliko wanamichezo wote duniani ndani ya kipindi hicho.

Messi ameingiza kiasi cha Pauni 100 milioni kwa mwaka huku akimtoa katika kiti hicho bondia maarufu wa Marekani, Floyd Mayweather ambaye alishika nafasi hiyo kwa miaka minne kati ya miaka saba iliyopita.

Messi aliingiza kiasi cha Pauni 72 milioni katika mshahara wake na bonasi za ushindi, wakati kiasi cha Pauni 28 kilichobaki kilitokana na mikataba yake ya kibiashara, wakati Ronaldo aliingiza kiasi cha Pauni 51 milioni kama mshahara na kiasi cha Pauni 35 milioni katika mikataba ya kibiashara.

Upande wa Neymar, yeye aliingiza Pauni 83 milioni huku mwanasoka mwingine anayefuata baada ya yeye akiwa ni Paul Pogba ambaye anashika nafasi ya 44 akiwa ameingiza kiasi cha Pauni 26 milioni.

Aliyeshika nafasi ya nne nyuma ya Messi, Ronaldo na Neymar ni Bondia wa Mexico, Canelo Alvarez aliyeingiza kiasi cha Pauni 74 milioni wakati mcheza tenisi maarufu wa Uswisi, Roger Federer akishika nafasi ya tano akiingiza kiasi cha Pauni 73.5 milioni.

Kukamilisha orodha ya 10 bora wengine waliofuata ni wachezaji mpira wa miguu wa Marekani (American Football) ambao ni Russell Wilson na Aaron Rodgers wote wakiingiza Pauni 70 milioni huku mastaa wa kikapu NBA, Le Bron James akiingiza Pauni 70 milioni, Stephen Curry ameingiza Pauni 63 milioni na Kevin Durant akiingiza Pauni 51 milioni.

Bondia wa Kiingereza, Anthony Joshua ambaye bado anaugulia maumivu ya kudundwa na bondia wa Mexico, Andy Ruiz Jr hivi karibuni anashika nafasi ya 13 huku akiwa Muingereza aliyeingiza pesa nyingi zaidi kando ya dereva wa Formula One, Lewis Hamilton, wote wakiwa wameingiza Pauni 43 milioni.

Mastaa wa Ligi Kuu ya England Alexis Sanchez (£24m), Mesut Ozil (£24m) na Mo Salah (£20m) ni miongoni mwa wanamichezo walioingia katika orodha ya 100 bora wakati nyota wa Real Madrid, Gareth Bale anashika nafasi ya 79 baada ya kuingiza kiasi cha Pauni 21 milioni.

Serena Williams aliyeingiza Pauni 23 milioni anakuwa mwanamke aliyeingiza kiasi kikubwa zaidi kwa mwaka wa fedha ambapo hata hivyo alishika nafasi ya 63. Mwaka mmoja uliopita hakukuwa na mwanamke aliyejitokeza katika orodha ya 100 bora.

Bosi mkuu wa Jarida la Fobres, Kurt Badenhausen alisema: “Kutanuka kwa soka duniani kote kumeonekana wazi katika mapato mwaka 2019, huku mastaa watatu wa soka Messi, Ronaldo, na Neymar wakiongoza katika orodha.

“Hata hivyo, kikapu kimeendelea kutawala katika 100 bora huku kukiwa na wanamichezo 35 ambao wameingiza kiasi cha Pauni 1 bilioni huku asilimia 72 ya kipato chao ikitokana na mishahara yao zaidi kuliko mikataba binafsi ya biashara.”

Orodha yao imejumuisha wanamichezo kutoka michezo 10 tofauti. NBA inaongoza (35), NFL (19) huku Baseball (15) soka wachezaji 12.

Kulikuwa na nchi 25 zilizotoa wanamichezo hawa matajiri tofauti na mwaka 2018 ambako kulikuwa na wanamichezo 22. Marekani imetawala ikiwa na wanamichezo 62 wakati Uingereza ilikuwa na wawakilishi watano ambao ni Joshua, Hamilton, Conor McGregor (£37m), Rory McIlroy (£31m) na Justin Rose (£25m).