Messi aongeza tuzo, Ronaldo ajivunia kiatu cha dhahabu

Muktasari:

Tangu waanze kukutana katika hafla za kukabidhana tuzo, wawili hao wamekuwa na maelewano mazuri, walionekana katika utulivu wa kirafiki, hakukuwa na hali ya mashaka mashaka ya kiushindani.

Katika toleo lililopita, mwandishi, Luca Caioli alizungumzia mchuano wa Ronaldo na Messi katika tuzo za Ballon d’Or akionyesha jinsi Ronaldo alivyotwaa tuzo ya tatu mwaka 2015 na kukaribia kumfikia Messi aliyekuwa na tuzo nne. Endelea…

“Anaangalia (mtoto wa Ronaldo) mechi zako (Messi) na kukuzungumzia wewe,” Ronaldo alimwambia Messi baada ya mastaa hao kukutana kabla ya hafla ya utoaji tuzo, tukio ambalo lilimfanya Ronaldo Junior, mtoto wa miaka minne wa Ronaldo akiwa hana la kusema.

Hadi hapo Ronaldo alikuwa ameshazifikia rekodi za tuzo za Ballon d’Or zilizowekwa na kina Cruyff, Van Basten na Platini ambao pia wamebeba tuzo hiyo mara tatu lakini sasa malengo yake kayahamishia kwa Messi, mpinzani wake ambaye ametwaa tuzo hiyo mara nne.

Hata hivyo badala ya kupunguza tofauti ya mataji, pengo hilo liliongezeka miezi 12 baadaye. Januari 11, 2016, Messi aliwasili mjini Zurich akiwa na matarajio makubwa ya kutwaa taji la tano la Ballon d’Or baada ya ukame wa miaka miwili.

Hata Ronaldo mwenyewe alikuwa akifahamu ukweli kwamba safari hiyo kulikuwa na mshindi asiye na shaka yoyote, na hakuwa yeye, “Sishangai kuwa hapa lakini Messi nafasi kubwa kwa sababu timu yake imeshinda mataji yote,’’ alikiri Ronaldo katika mkutano kabla ya hafla ya tuzo hiyo.

Tangu waanze kukutana katika hafla za kukabidhana tuzo, wawili hao wamekuwa na maelewano mazuri, walionekana katika utulivu wa kirafiki, hakukuwa na hali ya mashaka mashaka ya kiushindani.

Walikaa karibu katika hafla yenyewe na hakukuwa na mshangao pale mshindi alipotangazwa na pia hakukuwa na mtazamo wa kauli zenye kukinzana baina yao.

Messi alitwaa tuzo hiyo ya mwaka 2015 kwa asilimia 41 ya kura wakati Ronaldo alipata asilimia 27 na Neymar asilimia saba. Messi alipanda jukwaani kupokea tuzo kutoka kwa, Kaka, staa wa zamani wa AC Milan, Real Madrid na timu ya Taifa ya Brazil, Kaka alitwaa tuzo hiyo mwaka 2007.

Safari hii Messi hakuwa amevaa suti iliyozoeleka, alikuwa tofauti kidogo, aliiweka kando Dolce & Gabbana na badala yake akapiga suti aina ya Armani, alionekana katika mtazamo wa kiutu uzima zaidi, akiwa kama mwenye kutafakari mafanikio yake ya uwanjani.

“Hamasa na hali ya furaha inakufanya kupata tabu kidogo kuzungumza mbele ya umati wa watu,” alisema akiwa na tuzo mkononi mwake.

“Ni jambo zuri kwangu kushinda tuzo hii kwa mara nyingine baada ya miaka miwili ya kumshuhudia Cristiano (Ronaldo) akiibuka mshindi, ni jambo la kipekee hii kuwa tuzo ya tano, ni hatua kubwa mno, ni tofauti na ndoto yangu ya utotoni,” alisema kabla ya kuanza kutoa shukurani.

“Nataka kumshukuru kila mtu aliyenipigia kura, pamoja na wachezaji wenzake kwa sababu kama nisemavyo wakati wote kwamba hili lisingewezekana bila mchango wao, na nishukuru mchezo wa soka kwa kuniwezesha kupitia hatua hii, kwa mazuri na mabaya, kwa sababu yote hayo yamenisaidia kukua,’’ alisema Messi.

2009, 2010, 2011, 2012 na 2015, hakuna aliyewahi kupata mafanikio kama hayo na hakuna ambaye anatarajia kuna atakayeyafikia mafanikio hayo, lakini linapokuja suala la Messi ni kama vile hakuna cha kumzuia.

Ukiweka kando Ballon d’Or kuna mpambano mwingine mkali wa kuwania Kiatu cha Dhahabu Ulaya, ambacho tangu mwaka 1968, kumekuwa na utaratibu wa kumtangaza mfungaji wa mabao mengi wa ligi zote za juu za Ulaya.

Katika mpambano huo matokeo ni 4-3 (tangu kuchapishwa kitabu hiki 2015/16) na Ronaldo ndiye anayeongoza, ameshinda mwaka 2008 na Manchester United kwa mabao yake 31, akashinda tena na Real Madrid mwaka 2011 na mabao yake 40.

Ronaldo pia alishinda tena mwaka 2014 na mabao 31 na mwaka 2015 na mabao yake 48 pia akiwa na Real Madrid, hakuna aliyewahi kutwaa kiatu hicho mara nne na ni mchezaji pekee aliyebeba tuzo hiyo akiwa katika ligi za nchi mbili tofauti.

Wakati huo huo, Messi yeye alishinda mwaka 2010 kwa mabao 34, 2012 kwa mabao 50 na 2013 kwa mabao yake 46, yote hayo akiwa na klabu yake ya Barcelona. Katika eneo hilo kinara alikuwa ni Ronaldo.

Itaendelea Jumanne...