Messi anapangua tu rekodi za Uefa

BARCELONA, HISPANIA. SUPASTAA, Lionel Messi ameweka historia kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya juzi Jumanne baada ya kufunga kwenye ushindi wa mabao 5-1 iliyopata Barcelona dhidi ya Ferencvaros uwanjani Nou Camp.

Supastaa huyo wa Kiargentina mwenye umri wa miaka 33 amekuwa mchezaji wa kwanza kufunga bao kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa misimu 16 mfululizo wakati alipofunga bao la kwanza dhidi ya miamba hiyo ya Hungary.

Messi amefikia rekodi ya gwiji wa Manchester United, Ryan Giggs kutikisa nyavu kwenye michuano hiyo ya Ulaya kwa misimu 16 tofauti. Katika mchezo huo, mabao mengine ya Barcelona yalifungwa na Ansu Fati, Philippe Coutinho, Pedri na Ousmane Dembele. Mchezo ujao, Barca itawafuata Juventus.