Messi, wenzake waamriwa kurudisha magari

Tuesday July 23 2019

 

BARCELONA,HISPANIA .KAMPUNI ya magari ya AUDI imewataka mastaa wa Barcelona wakiongozwa na Lionel Messi kurudisha magari waliyopewa na kampuni hiyo baada ya mkataba wa udhamini kati ya kampuni hiyo na Barcelona kukoma.

Messi pamoja na mastaa wengine wa Barcelona walipewa fursa ya kuchagua magari ya kifahari ya AUDI wanayoyataka baada ya kampuni hiyo kutoka Ujerumani kuingia katika ushirikiano wa kibiashara na Barcelona mwaka jana.

Messi alichagua gari aina ya Audi RS 6 Avant yenye thamani ya Pauni 130,000 wakati kiungo wa kimataifa wa Croatia, Ivan Rakitic ambaye hatima yake bado ipo shakani Nou Camp aliamua kuchagua gari aina ya Audi Q7 yenye thamani ya pauni 65,000.

Lakini, sasa kampuni hiyo imeyataka magari hayo katika yadi yake baada ya kumaliza mkataba na mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Hispania tangu Juni 30, mwaka huu na imewapa wiki tatu tu mastaa hao kurudisha magari hayo ya kifahari.

Wachezaji hao wamekuwa wakiyatumia magari hayo kwa safari za kila siku kwenda na kurudi katika uwanja wa mazoezi Ciutat Esportiva Joan Gamper uliopo kando ya Jiji la Barcelona, ingawa baadhi wamekuwa wakitumia magari binafsi.

“Mwaka jana, mmoja kati ya mabosi wa kampuni hiyo ya Audi, Christian Guenthner alikaririwa akisema “Kwa shughuli maalum za kibiashara wanatumia magari ya Audi. Wakati wa kuchagua magari hayo kampuni na klabu zilishirikiana kwa karibu zaidi.

Advertisement

“Wachezaji wanaweza kuchagua magari yoyote mazuri zaidi, kuanzia madogo kwa ajili ya wachezaji chipukizi. Wanapewa fursa ya kuchagua magari ya aina mpya yenye mambo mengi mapya. Na kwa fasheni yetu mpya ya magari watapata mambo mengi zaidi.”

Kumalizika kwa mkataba huo kunafuatia miaka 13 ya uhusiano kati ya kampuni hiyo ya Ujerumani na klabu hiyo ya Catalunya, ambayo pia imekuwa ikifanya ushirikiano kama huo na klabu nyingine mbili kubwa za Ulaya Real Madrid na Bayern Munich.

Kila mwaka wachezaji wamekuwa wakipewa aina mpya za magari huku Audi ikiuza magari ambayo wanayarudisha kwa watu wengine. Katika kikosi cha sasa cha Barcelona, kiungo mkabaji, Sergio Busquets ndiye alichukua gari la thamani zaidi. Gari lake aina ya Audi R8 Coupe V10 lilikuwa na thamani ya Pauni 192,000.

Guenthner aliweka wazi suala la watu wengine kuruhusiwa kununua magari hayo yaliyokuwa yakitumiwa na mastaa hawa akisema; “Kuna nafasi yoyote ya kununua moja kati ya magari haya baada ya wachezaji kuyatumia? Ndio, inawezekana kupata moja kati ya magari haya kutoka katika soko la magari yaliyotumika”.

Magari ya Audi ya wachezaji wa Barcelona na thamani zake

Marc-Andre ter Stegen Audi SQ5 TFSI Mythos black (£71,000)

Nelson Semedo Audi Q7 Carrara white (£75,000)

Gerard Pique Audi RS 6 Avant performance Daytona gray (£127,000)

Ivan Rakitic Audi Q7 Graphite gray (£65,000)

Sergio Busquets Audi R8 Coupe V10 plus Daytona gray (£192,000)

Luis Suárez Audi RS 6 Avant performance Daytona gray (£127,000)

Lionel Messi Audi RS 6 Avant performance Sepang blue (£127,000)

Ousmane Dembele Audi RS3 Sportback Panther black (£56,000)

Philippe Coutinho Audi Q7 3.0 TDI (£65,000)

Jordi Alba Audi Q7 Sepang blue (£65,000)

Sergi Roberto Audi RS3 Sportback Catalunya red (£56,000)

Samuel Umtiti Audi RS3 Sportback Catalunya red (£56,000)

Ernesto Valverde Audi Q7 e-tron quattro Florett silver (£65,000).

Advertisement