Messi, mabosi Barca watibuana

Muktasari:

Alhamisi ya juma lililopita, Bartomeu alipendekeza kuwa Barcelona inafikiria kupunguza mishahara ya waajiriwa wake wote kuanzia bodi hadi wachezaji. Undani wa mpango huo haukuwekwa bayana, lakini Messi na mastaa wengine hawakuubariki.

BODI ya Barcelona ni sawa na mfu anayetembea kwa sasa. Tangu ianze kulumbana na nyota wake Lionel Messi, hali haijawa sawa ndani ya bodi. Kuanzia iliporipotiwa kuwa Barcelona ina mpango wa kuwakata wafanyakazi wake mishahara, hali ya hewa ilichafuka.

Tetesi za kuchangia kuondoka kwa Neymar. Kukwaruzana na Eric Abidal. Kudaiwa kushinikiza kurejeshwa kwa Xavi na Carles Puyol warudishwe klabuni katika nafasi ya menejimenti, ni baadhi ya viashiria vya kuwepo kwa upepo mbaya kati ya Messi na Bodi ya Barcelona.

Mapema wiki iliyopita, Lionel Messi alidaiwa kubatukiana na Bodi ya Barcelona, kuhusu pendekezo la wachezaji kukatwa mishahara. Messi aliiambia bodi kuwa yeye na wenzake wako tayari kukatwa mishahara yao kwa asilimia 70.

Lakini pia, anadaiwa kuikosoa bodi kwa jinsi walivyoshughulikia suala la maambukizi ya virusi vya corona. Hii ndio vita mpya kati ya Muargentina huyo na uongozi wa Rais Josep Bartomeu. Lakini nani ni mbaya katika hili? Hilo ni swali linaloumiza vichwa vya wengi kote duniani.

Alhamisi ya juma lililopita, Bartomeu alipendekeza kuwa Barcelona inafikiria kupunguza mishahara ya waajiriwa wake wote kuanzia bodi hadi wachezaji. Undani wa mpango huo haukuwekwa bayana, lakini Messi na mastaa wengine hawakuubariki.

Inashangaza sana maana haiingi akilini kwa mtu aliyetajwa na Shirikisho la Soka Ufaransa, kama mchezaji mwenye mshahara mkubwa zaidi (Pauni 116 milioni au euro 131 milioni) kwa mwaka akatae kukatwa mshahara wake kuchangia vita dhidi ya janga la corona?

Messi na mastaa wengine kugoma kabisa kukubaliana na wazo la kusaidia, huku akiendelea kukaa kimya asijitokeze kuchangia kama walivyofanya wengine kabla ya kuibuka hivi majuzi kuchangia Pauni 900,000 (Euro 1 milioni) katika hospitali mbili za Catalonia na Argentina.

Siku ya Jumatatu kupitia mtandao wa Instagram, aliibuka na kutoa kauli ambayo ilionyesha wazi kuwa kuna jambo linaloendelea chini ya kapeti pale Camp Nou. Katika ujumbe huo, mshindi huyo mara sita wa Ballon d’Or aliandika: “Inashangaza kuwa ndani ya klabu kuna kundi la watu wanaojaribu kulazimisha wachezaji na wafanyakazi kufanya watakavyo. Inakera zaidi kuwekewa presha na baadhi ya watu kufanya kitu ambacho wewe mwenyewe ulikuwa tayari kukifanya kwa hiari yako.”

Kwa ufupi ni kwamba, kwa mujibu wa maneno ya Messi, bodi ilikuwa inajaribu kuwafunga wachezaji kamba kitu ambacho kwao waliona sio sawa. Wakati Messi akiandika hayo, katika upande wa pili wa sarafu kulikuwa na kikao cha marais wote wa La Liga. Taarifa zinasema kuwa, katika kikao hicho kilichoendeshwa kwa njia ya mtandao, ajenda kubwa ilikuwa ni namna ya kukabiliana na changamoto za kiuchumi inayochangiwa na janga la corona linaloendelea kuiandama dunia. Unaambiwa marais na wakurugenzi kadhaa walijikuta wakishindwa kufuatilia kikao kwenye laptop zao (kwa njia ya vedeo) na badala yake kuhamishia mawazo yao kwenye simu zao kusoma ujumbe wa Whatsapp wa ‘Wow! umeona alichoandika Messi?’

Kilichofuata ni Bodi ya Barcelona kuhaha kujieleza. Fasta klabu ikatoa taarifa na magazeti mawili ya michezo ya Catalan yakachapisha habari kuhusu mkutano wa waandishi wa habari, siku iliyofuata Bartomeu akauhakikishia umma kuwa wako pamoja na wachezaji.

Hata hivyo, katika taarifa yake hiyo, Bartomeu alitamka maneno ambayo yalionyesha wazi kuna tatizo. Alisema: “Inawezekana wamekasirishwa (wachezaji) na kauli za watu kutoka ndani na nje ya uwanja bila ya kufahamu undani wa mambo.”

Huko kukiri tu kuwa wachezaji walikuwa na haki ya kukasirika, kumeonesha kuwa Bartomeu mwenyewe anatambua kuwa hali sio shwari klabuni. Aidha, ilitosha kuthibitisha ni kwanini wachezaji walikuwa tayari kukatwa wao mishahara na si wafanyakazi wengine. Hii sio mara ya kwanza Bodi ya Barcelona imeonekana kuyumbishwa kimaamuzi. Hivi karibuni ilishuhudiwa jinsi Messi alivyombwatukia hadharani mkurugenzi wa Michezo, Eric Abidal aliyewahusisha wachezaji na kuondoka kwa Kocha Ernesto Valverde.

Safari hii wachezaji wakiishukia bodi kutokana na kile walichodai ni bodi kuwa na haraka ya kuidhinisha mpango wa ERTE ambao ni utaratibu wa kuwakata wafanyakazi mishahara na kuwafuta wengine kazi kwa muda.

Wakati huko Camp Nou mambo yakiwa hivyo, Santiago Bernabue hawana hilo wazo. Inadaiwa kuwa Real Madrid bado haijafikiria kuwakata mishahara wafanyakazi wake, jambo linalowafanya mastaa wa Barcelona kuihoji bodi kwa nini wana haraka ya kufanya hivyo.

Sio Madrid tu, hata huko Espanyol ambayo ni moja ya klabu za Catalonia inadaiwa kuwa mpango huo unahusu wachezaji tu. Tetesi zinasema kuwa bodi inataka kuchukua uamuzi huo kutokana na malengo waliyojiwekea mwanzoni mwa msimu. Barcelona ilikuwa imepanga kuingiza kiasi cha Pauni 106 milioni, lakini kutokana na janga hili ni wazi kuwa hilo halitawezekana. Pia kulikuwa na mpango wa kutumia Pauni 620 milioni (Euro 700 milioni) kwa ajili ya ukarabati wa Camp Nou. Hilo nalo ni ngumu kwa sasa.

Tetesi zinasema kuwa, Messi hakufurahishwa na uamuzi wa kumuuza Neymar (2017). Philippe Coutinho na Ousmane Dembele walikuja kuchukua nafasi yake, lakini bado Messi hakuridhika na alitaka klabu imrudishe Neymar, ila badala yake iliamua kumleta Grizmann. Muargentina huyo ana ndoto ya kuwa sehemu ya timu ya ushindi kabla ya kutundika daluga na anaonyesha wazi kutokuwa na imani kuwa bodi ya sasa itawezesha hilo kutimia. Kabla ligi hazijasimama kutokana na hofu ya corona, kulikuwa na dalili ya msimu kutowaendea poa Barcelona.

Walikuwa mbioni kuteleza kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara nyingine. Messi mwenyewe alikuwa ameshakiri kuwa hawakuwa katika nafasi nzuri ya kushinda ubingwa wa Ulaya. Mbaya zaidi haonyeshi nia ya kuongeza mkataba.

Mwisho wa yote hayo, ingekuwa ni presha ya kuitaka bodi kuachia ngazi.