Messi, Ronaldo waweka rekodi timu za Taifa

Wednesday June 26 2019

 

KATIKA toleo lililopita mwandishi Luca Caioli alichambua hali ilivyokuwa katika fainali za Kombe la Dunia 2010 hasa kisa cha Cristiano Ronaldo kuzomewa na mashabiki ambao walikuwa wakijiuliza kulikoni staa akiwa na timu ya Ureno hachezi vizuri kama anavyocheza akiwa na timu ya Real Madrid. Endelea…

Yote kwa yote alichokionyesha Ronaldo ilipotolewa Ureno hakikutoa ishara nzuri na vyombo vya habari havikuliacha tukio hilo libali hivyo hivyo.

Vilimkosoa mchezaji huyo na pia alijikuta akishutumiwa, kila mmoja Ureno alitaka kufahamu kwa nini Ronaldo hachezi katika timu ya Taifa ya Ureno kama anavyocheza akiwa na Real Madrid.

Ni tukio ambalo Messi naye analijua fika, kuwa katika mazingira kama hayo ya kukosa msaada katika jambo ambalo huwezi kuelezea ni kwa nini liko jinsi lilivyo.

Miaka miwili baadaye katika fainali za Euro 2012, Ronaldo akawa mtu wa mashabiki, Juni 27, 2012 Ureno ikatolewa na Hispania katika fainali hizo kwenye hatua ya nusu fainali. Lakini safari hii mashabiki nyumbani walimpokea vizuri.

Kiwango chake cha uchezaji na tabia zake wakati wote wa fainali hizo ilikuwa tofauti na hakuna aliyekuwa na hofu naye nyumbani. Ronaldo ni bora duniani.

Advertisement

Hata hivyo mafanikio hayo hayakuwa na maana mwaka 2014 yaani miaka miwili baadaye kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini Brazi, Ureno ilitolewa katika hatua ya makundi ikiwa ni mara ya kwanza tangu mwaka 2002 na katika fainali hizo Ronaldo alifunga bao moja tu.

Ukweli ni kwamba mambo yalikuwa magumu kwake hasa baada ya kupitia msimu mgumu na uliojaa uchovu na klabu yake ya Real Madrid, vyombo vya habari viliendelea na shutuma zake kama kawaida lakini safari hii timu ilikuwa kitu kimoja.

“Tunarudi nyumbani tukiwa wenye furaha, tumejaribu kadri ya uwezo wetu lakini soka ndivyo lilivyo,’’ alisema Ronaldo baada ya Ureno kutolewa.

Amecheza fainali tatu za Kombe la Dunia na kwa mara ya kwanza ndoto zake ameshindwa japo kuzisogelea, amecheza kwa dakika 1,114, mechi 13 na kufunga mabao matatu, walau anaweza kujifariji kwa kuwa kinara wa mabao katika historia ya Ureno kwa mabao yake 61.

Hadi wakati wa fainali za Kombe la Dunia 2018 nchini Urusi, Ronaldo alifikisha umri wa miaka 33 na ingawa alicheza katika fainali hizo, lakini baada ya fainali za 2014 hakuna ambaye aliweza kufahamu hatima yake ingekuwaje.

Kwa upande mwingine hadi wakati huo mpinzani wa Ronaldo, Messi naye tayari akili yake alikuwa ameiweka Urusi kwenye fainali za 2018 mara tu baada ya fainali za 2014 Brazil kufikia ukomo katika tukio la kukatisha tamaa baada ya kufikia hatua ya fainali na kushindwa kufurukuta mbele ya Ujerumani.

Pamoja na matokeo hayo ya kusikitisha, Messi naye ni kama Ronaldo, aliibuka mfungaji bora wa kihistoria wa Argentina kwa mabao yake 55 akiivunja rekodi ya Gabriel Batistuta ambaye aliichezea Argentina kuanzia mwaka 1991 hadi 2002.

Lakini pia alikuwa na medali ya dhahabu kupitia timu ya Taifa ya Argentina ambayo iliibwaga Nigeria katika fainali za Michezo ya Olimpiki zilizofanyika Beijing, China mwaka 2008 kwa bao pekee la Angel Di Maria.

Katika michezo hiyo ya Olimpiki, mechi inayokumbukwa zaidi ni ile ya nusu fainali dhidi ya Brazil ambayo imeendelea kuwa katika historia kwa namna ambavyo Argentina iliibwaga na kuidhalilisha Brazil kwa mabao 3-0.

Ni kipigo ambacho kama kilitoa ishara ya mabadiliko na mwanzo mpya, ilikuwa kama vile zama za Ronaldinho zinafikia ukingoni na mwanzo mpya wa Messi asiyekuwa na mpinzani ukianza kuibuka.

Mara baada ya mechi hiyo kumalizika, Ronaldinho alijikuta akipozwa na rafiki na kiongozi wake Messi ambaye alimuwekea mkono mabegani katika kumfariji.

Ni picha ambayo ilitoka katika magazeti karibu yote ya siku iliyofuata, picha iliyoonyesha ni namna gani dunia ya soka inaweza kuwa kitu chenye mfano wa ukatili.

Itaendelea Jumamosi ijayo

Advertisement