Messi: Kikubwa ushindi, kiwango achana nacho

Muktasari:

Nyota wa FC Barcelona, Lionel Messi ameiongoza timu yake ya taifa la  Argentina  kuibuka na ushindi kwenye mchezo wa kuwania nafasi ya  kufuzu kombe la Dunia dhidi ya Ecuador.

RIO GRANDE, ARGENTINA. LIONEL Messi amezungumzia umuhimu wa ushindi na sio kiwango ambacho timu yao ya taifa la Argentina wamekionyesha kwenye mchezo wao wa kuwania nafasi ya  kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Ecuador.

Messi alikuwa shujaa kwenye mchezo huo kwa mara nyingine baada ya kuiongoza Argentina kuibuka na ushindi wa bao 1-0 alilofunga kwa mkwaju wa penalti, ikiwa ni mchezo wake wa kwanza tangu Novemba mwaka jana.

"Tulijua itakuwa ngumu. Lakini zaidi jambo muhimu ni kwamba tulishinda na sasa lazima tufanye kazi ya ziada  ili kuendelea kuwa bora.

"Ilikuwa muhimu kuanza na ushindi kwa sababu siku zote huwa ni ngumu  kufuzu kombe la Dunia. Mechi huwa ngumu kila wakati. Tulitumai kiwango cha uchezaji wetu kingekuwa tofauti kwa sababu hatujacheza pamoja karibu mwaka mzima," amesema.

Messi na wachezaji wenzake wa timu ya taifa la Argentina walicheza mchezo huo nyumbani huku uwanja ukiwa mtupu kutokana na janga la virusi vya corona ambalo linaendelea kutikisa Dunia.

"Umekuwa mwaka mgumu ambao tunauishi. Tulipenda kucheza mbele ya mashabiki wetu na kuwapa furaha," amezungumza Messi ambaye Jumanne ataiongoza tena Argentina kucheza dhidi ya Bolivia.

Michezo mingine ambayo ilichezwa ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia kutoka Amerika Kusini, ilishuhudiwa Paraguay ikitoka sare ya mabao 2-2 dhidi Peru huku Uruguay ikiifunga Chile mabao 2-1.