Messi, Cavani wataka kuzichapa uwanjani

Muktasari:

Washambuliaji Lionel Messi na Edinson Cavani nusura wazichape kavukavu baada ya kutoleana maneno makali katika mchezo wao wa kirafiki uliochezwa jana jioni.

Tel Aviv, Israel. Lionel Messi na Edinson Cavani nusura wazichape uwanjani baada ya kutokea mzozo baina yao katika mchezo kati ya Argentina na Uruaguay.

Messi na Cavani walitoleana maneno makali katika mchezo huo wa kirafiki ambao timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2

Kwa mujibu wa gazeti la Ole la Argentina lilisema Messi alimjibu Cavani yuko tayari kupigana naye baada ya Cavani kumtishia atampiga.

Washambuliaji hao nguli walitenganishwa na beki wa Uruaguay Diego Godin baada ya kutoleana maneno makali huku kila mmoja akijiandaa kumvaa mwenzake.

Marudio ya mkanda wa video unamuonyesha Cavani akimpiga kiwiko Messi katika harakati za kuwania mpira.

“Ilikuwa mechi ngumu yenye kila aina ya ushindani, ulikuwa mchezo wenye kasi timu zote zilicheza kwa umakini,”alisema Cavani.

Mshambuliaji huyo wa Paris Saint Germain (PSG) alisema mchezo huo ulizikutanisha timu zinazotoka Amerika.

Messi aliiokoa Argentina baada ya kufunga bao la kusawazisha dakika za majeruhi. Bao jingine lilifungwa Sergio ‘Kun’ Aguero.

Mabao ya Uruguay katika mchezo ambao Argentina ilitawala sehemu kubwa yalifungwa na Cavan, Luis Suarez.