Mendy hawezi kuwa Drogba wa makipa

SIKILIZA wasifu wa watu hawa wawili. Jina? Edouard Osoque Mendy. Tarehe ya kuzaliwa? Machi Mosi, 1992. Miaka? 28. Mahala pakuzaliwa? Montivilliers nchini Ufaransa. Timu ya taifa? Senegal.

Huyu ndiye kipa mpya wa Chelsea lakini sikiliza wasifu wa kipa mwingine. Huyu hapa. Jina? Andre Onana. Tarehe ya kuzaliwa? April 2, 1996. Miaka? 24. Mahala pakuzaliwa? Nkol Ngok nchini Cameroon. Timu ya taifa? Cameroon.

Sitaki kuwa mbaguzi sana lakini kuna kitu nimeendelea kugundua. Makipa wa Afrika hawaaminiwi sana Ulaya. Nadhani kuna mahala wazungu wa timu kubwa wameamua kutowaamini makipa wa Bara la Afrika.

Mendy amejiunga na Chelsea akiwa kipa wa kwanza kutoka Afrika kucheza katika timu kubwa kama Chelsea. Kabla ya hapo bado hatujaona makipa wa Afrika wakidaka katika klabu kubwa za Ulaya kama Barcelona, Real Madrid, Arsenal, Manchester United, Juventus, Bayern Munich na nyinginezo.

Lakini subiri kwanza. Mendy amezaliwa wapi? Ulaya. Inawezekana ndio maana Chelsea wamemwamini kumpa nafasi na kuna uwezekano mkubwa akachukua nafasi ya Kepa Arrizabalaga. Kama angezaliwa Afrika wangemuamini? Sina uhakika.

Kipa wa Afrika aliyeaminiwa kudaka timu kubwa Ulaya alikuwa ni Bruce Globbelaar. Aliwahi kutamba katika lango la Liverpool miaka ya themanini. Subiri kwanza? Kumbe alikuwa mzungu. Inawezekana ndio maana walimwamini.

Nimegundua wazungu hawatuamini sana katika nafasi hii hasa kama tumezaliwa Afrika moja kwa moja.

Kwa nini Onana hakununuliwa na timu kubwa licha ya kutamba sana na Ajax katika miaka ya karibuni? Aliifikisha Ajax nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya misimu miwili iliyopita na kuanzia hapo amekuwa akihusishwa kwenda timu kubwa bila ya mafanikio.

Amewahi pia kuhusishwa sana na Chelsea lakini Mendy ametoka kusikojulikana na kuingia Chelsea.

Sio kwamba Waafrika hatuaminiwi kabisa katika nafasi hiyo lakini inawezekana kuna mambo mengi nyuma yake.

Labda hatupeleki wachezaji wengi wa nafasi hiyo. Labda pia kuna kitu tunakikosa kimbinu katika kuhimili mikiki ya nafasi hiyo huko kwa wakubwa wa Ulaya.

Cameroon ndio nchi ambayo imetoa makipa wengi waliocheza Ulaya walau kwa mafanikio ingawa hawakuwahi kugusa timu kubwa. Kipa wa mwisho kabisa wa Cameroon kutamba Ulaya alikuwa Idrisou Kameni. Huyu alicheza Ufaransa kabla ya kuibukia Espanyol, Malaga na Fenerbahce.

Kabla yake walikuwepo watu wazito lakini hawakugusa timu kubwa. Alikuwepo Jacues Sang’oo. Huyu alicheza Ufaransa klabu za Canon Yaoundé ya kwao Ufaransa kabla ya kwenda Ufaransa kucheza klabu za Toulon, Le Mans na Metz kisha akatimkia Deportivo La Coruña ya Hispania.

Baadaye akaja mzee wetu wa zamani, Joseph Antoine Bell. Huyu aliingia Ulaya mwaka 1985. Akacheza zaidi Ufaransa katika klabu za Marseille, Toulon, Bordeaux na Saint-Étienne. Hakuweza kugusa Bayern Munich, Juventus, Manchester United wala kwa wakubwa wengine.

Kuna mtu aliitwa Thomas N’kono. Mmoja kati ya makipa bora kuwahi kutokea barani Afrika. Huyu ndiye alikuwa kipa namba moja wa timu ya taifa ya Cameroon katika fainali za kombe la dunia nchini Italia mwaka 1990.

Alionyesha kiwango kikubwa kiasi kwamba kipa mahiri wa sasa wa Italia, Gigi Buffon aliamua kumuita mwanae jina la Thomas ikiwa ni heshima yake kwa N’Kono. Buffon alikuwa kijana muokota mipira katika fainali za kombe la dunia mwaka 1990 na alivutiwa mno na N’kono kiasi kwamba aliamua kumpa mwanae jina la Thomas.

Hata hivyo, licha ya umahiri huu lakini N’kono aliishia kucheza katika klabu ya Espanyol tu ya Hispania. Hakuwahi kugusa katika timu kubwa zaidi ya hii. Klabu nyingine alizocheza zilikuwa za kawaida tu. kuna jambo kwa makipa wa Afrika.

Pia mkumbuke kipa aliyeitwa, Tony Silva. Wengi tunamkumbuka kwa kuwa kipa namba moja wa Senegal katika fainali za kombe la dunia nchi za Korea Kusini na Japan mwaka 2002.

Huyu alizaliwa Afrika na kucheza sana Ufaransa katika klabu za Monaco na Lille ambazo alicheza kwa misimu nane. Hakuweza kwenda juu zaidi ya hapo.

Wakati Waafrika tukiendelea kujivunia mastaa wakubwa waliopita katika nafasi mbalimbali katika timu kubwa za Ulaya, mambo bado ni mazito kwa makipa.

Sijui kwanini hawatumiani. Tuna matatizo ya kiufundi? Sijui. Ni wafupi? Hapana. Akina N’kono walikuwa warefu kama hawa akina Manuel Nauer. Tunapeleka makipa wachache Ulaya? Sina uhakika. Katika madaraja ya kawaida wapo wengi Ulaya. Tatizo nini? Sijui.

Vyovyote ilivyo mpaka sasa Afrika haijatoa Samuel Eto’o wa upande wa makipa. Haijatoa Didier Drogba wa upande wa makipa. Haijatoa Nwankwo Kanu wa upande wa makipa. Haijatoa kipa ambaye ametokea katika vurugu za mtaani Afrika na kwenda kuwa kipa mkubwa wa timu kubwa barani Ulaya.

Hata kama Mendy atafanya mambo makubwa pale Stamford Bridge kumbuka kwamba vurugu zake za utotoni alizianzia katika kitanda cha hospitali pale Paris.

Hakuanzia huku Dakar, Lagos wala Yaoundé. Ameanzia kwa wazungu kwahiyo hawezi kuwa Drogba wa makipa.

Nilikuwa natamani Onana afike mbali zaidi. Alianzia timu ya vijana ya Barcelona kisha akaibukia Ajax. Baada ya kutamba na Ajax nilitazamia klabu kubwa kubwa za Ulaya zimchukue lakini mpaka sasa anasota pale Ajax.

Wakati akina Hakim Ziyechi, Donny van de Beek, Matthijs de Ligt, Frenkie de Jong na wengineo wameondoka, yeye bado anasota pale pale. Ni kwa sababu ni kipa aliyezaliwa Afrika? Au kuna jambo jingine tofauti ambalo Wazungu wameliona?