Mendes aongoza mawakala wa wachezaji kwa mkwanja

SOKA la kisasa haliwezi kukamilika bila ya kuwapo na mawakala wa wachezaji. Kilichopo ni kwamba huwezi kusajili mchezaji yeyote wa maana bila ya kupitia wakala na wachezaji wote mahiri wapo na mawakala wao ambao wamekuwa wakihangaika kuwatafutia dili za maana kwenye timu mbalimbali.

 

IN SUMMARY

  • Hii hapa ndio orodha ya mawakala watano waliopiga pesa nyingi kutokana na malipo waliyopata kwenye biashara walizofanya kuuza wachezaji. Hivi ndivyo vipato vyao kwa shughuli hiyo ya kuuza wachezaji.

Advertisement

SOKA la kisasa haliwezi kukamilika bila ya kuwapo na mawakala wa wachezaji. Kilichopo ni kwamba huwezi kusajili mchezaji yeyote wa maana bila ya kupitia wakala na wachezaji wote mahiri wapo na mawakala wao ambao wamekuwa wakihangaika kuwatafutia dili za maana kwenye timu mbalimbali. Hii hapa ndio orodha ya mawakala watano waliopiga pesa nyingi kutokana na malipo waliyopata kwenye biashara walizofanya kuuza wachezaji. Hivi ndivyo vipato vyao kwa shughuli hiyo ya kuuza wachezaji.

5.Mino Raiola- Pauni 18.7 milioni

Sifa moja kubwa ya Mino Raiola ni kwamba amekuwa wakala wa wachezaji wengi watukutu. Kitendo cha kuweza tu kuwamiliki wachezaji kama Mario Balotelli na Zlatan Ibrahimovic kimeelezwa kuwa ni kitu kikubwa sana kutokana na akili za wachezaji hao. Lakini, Raiola ana wachezaji wengine wa maana pia kwenye orodha yake ambao wanamfanya kupiga pesa ndefu zinazomfanya awe na maisha matamu. Wakala huyo amedaiwa kuwa na kipato cha Pauni 18.7 milioni alichovuna kwenye dili za kuwauza wachezaji tu, achana na biashara nyingine anazofanya. Baadhi ya wachezaji wake ni Paul Pogba, Henrikh Mkhitaryan, Blaise Matuidi, Zlatan Ibrahimovic, Romelu Lukaku, Mario Balotelli na kipa Gianluigi Donnarumma.

4.Jose Otin- Pauni 19.2 milioni

Ukimweka kando Jorge Mendes, wakala mwingine anayeshikilia mastaa wa maana huko Hispania ni Jose Otin. Wakala huyo anamiliki wachezaji wengi sana wa Kihispaniola na hivyo kuripotiwa kwamba amevuna kiasi cha Pauni 19.2 milioni kama malipo yake kutokana na kukamilisha dili mbalimbali za mchezaji kutoka timu moja kwenda nyingine. Baadhi ya wachezaji wake matata kabisa wa Kihispaola anaowasimamia ni pamoja na Vitolo, Fernando Torres, Javi Martinez, Jesus Navas, Pedro, Raul Garcia na Nacho Monreal.

3.Volker Struth- Pauni 27.8 milioni

Kama kuna klabu yoyote inahitaji kusaini mchezaji wa kutoka kwenye Bundesliga basi hakuna shaka anahitaji kuwa na namba ya simu ya wakala Volker Struth. Ndiye anayeshikilia vichwa vya maana vya wachezaji wanaotamba kwenye ligi hiyo ya Ujerumani na dili zake alizofanya zimeripotiwa kumwingizia mkwanja mrefu, Pauni 27.8 milioni. Baadhi ya wachezaji anaowasimamia ni pamoja na Marco Reus, Mario Gotze, Toni Kroos, Benedikt Howedes, Sidney Sam, Omer Toprak, Gonzalo Castro na Josip Drmic.

2.Jonathan Barnett- Pauni 28.8 milioni

Kwa wachezaji wa Kingereza hakuna mtu anayejua kupiga dili za maana kama wakala Jonathan Barnett. Ndiye aliyehusika kwenye kumuuza Gareth Bale kwa pesa ndefu kwenda Real Madrid. Barnett ameripotiwa kuvuna Pauni 28.8 milioni katika shughuli zake za kuwatafutia timu wachezaji na wakali ambao anawasimamia ni pamoja na Bale, Joe Hart, Wojciech Szczesny, Scott Sinclair, Luke Shaw, Rafael, Glen Johnson, Phil Jagielka, Adam Lallana, Ashley Cole, Sylvain Distin, Patrick Roberts na Richard Wright.

1.Jorge Mendes- Pauni 62.8milioni

Jorge Mendes hakuna ubishi ndiye wakala wa wachezaji maarufu na tajiri zaidi duniani. Wakala huyo amedaiwa kuvuna Pauni 62.8 milioni kutokana na shughuli zake katika kuwauza wachezaji. Baadhi ya mastaa anaowasimamia ni Cristiano Ronaldo, James Rodriguez, Eliaquim Mangala, Pepe, Ricardo Carvalho, Fabio Coentrao,Diego Costa, Thiago Silva, Tiago, Radamel Falcao, Angel di Maria, David de Gea na kocha Jose Mourinho.

More From Mwanaspoti
This page might use cookies if your analytics vendor requires them. Accept