Media FC sasa kufanya kweli

Muktasari:

 

  • Naye aliyekuwa nahodha wa Bandari FC, Patrick Wanyama alisema wanatarajia kucheza mechi za kirafiki katika sehemu mbalimbali za Mombasa na Mkoa wa Pwani kwa minajili ya kuonyesha jinsi walivyokuwa wakisakata soka hapo zamani.

MOMBASA .Kocha Mkuu wa Coast Media FC, Kevin Odit amesema japo kazi yao ni kuandika ama kusoma habari, lakini sasa wamepania kuhakikisha baadhi yao wanacheza soka la hali ya juu na timu yao hiyo inakuwa mojawapo ya zile zinazotajika.

Akizungumza baada ya mechi ya kirafiki dhidi ya Bandari Old Guards katika Uwanja wa Mbaraki Sports Club, Odit alisema wameanza kucheza mechi za kirafiki kwa ajili ya kuiamrisha kikosi walichonacho katika safari yao ya kufika mbali katika soka la Mkoa wa Pwani.

“Nina imani kubwa kwa jinsi tulivyocheza na Bandari Old Guards ambayo wachezaji wake wanafanya mazoezi kila siku na kutoka sare, tumeonyesha tunaweza na tutafika mbali baada ya kujitayariosha kwa mazoezi,” alisema mkufunzi huyo.

Aliyekuwa straika wa Bandari FC miaka iliyopita, Athuman ‘Lineker' Mbuggus alisema wanajivunia kutoka sare na timu ya Coast Media ambayo aliisifu kuwa timu yenye chipukizi wenye kulisakata soka la hali ya juu.

“Tumetoka sare na timu yenye wanasoka chipukizi wenye vipaji na tumejitahidi na kukataa kushindwa kwani tumeonyesha ubora wetu kutokana na kuwa huwa tunafanya mazoezi ya pamoja kila siku,” alisema Mbuggus.

Naye aliyekuwa nahodha wa Bandari FC, Patrick Wanyama alisema wanatarajia kucheza mechi za kirafiki katika sehemu mbalimbali za Mombasa na Mkoa wa Pwani kwa minajili ya kuonyesha jinsi walivyokuwa wakisakata soka hapo zamani.