Mechi ya Yanga yawakosesha amani mashabiki Simba

Muktasari:

Ushindi wa mechi ya 17 saba kati ya 19 walizocheza imeelezwa kuwa ni mtego wa maana ambao ni lazima Simba itakaporudi kwenye majukumu ya kitaifa, itapata tabu ikiwa na presha kubwa, jambo linaloweza kuwaacha mbali zaidi katika harakati za kusaka ubingwa.

NI kweli maisha wakati mwingine hayana usawa, lakini unaambiwa Simba ikiwa imepaa kwenda nje ya nchi kucheza mechi za kimataifa, watani zao Yanga wapo pale Shinyanga kwa ajili ya mchezo wa wa Ligi Kuu Bara, huku wakiwatega kijanja vijana wa Msimbazi.

Ushindi wa mechi ya 17 saba kati ya 19 walizocheza imeelezwa kuwa ni mtego wa maana ambao ni lazima Simba itakaporudi kwenye majukumu ya kitaifa, itapata tabu ikiwa na presha kubwa, jambo linaloweza kuwaacha mbali zaidi katika harakati za kusaka ubingwa.

Makocha na wadau mbalimbali wa soka, wametoa maoni yao jinsi klabu hizo mbili zilivyoachana kwenye alama walizonazo mpaka sasa na kusema, Simba itakuwa na presha na kazi kubwa kuhakikisha inavitumia vyema viporo vyao kuwafukuza watani.

Nyota wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua alisema licha ya ubingwa kuonekana una muelekeo wa kutua Jangwani, lakini katika soka lolote linawezekana, lakini ili Simba itetee taji lazima waombee Yanga apoteze, kitu kinachoweza kuwa kigumu.

Hata hivyo Chambua alisema Yanga haipaswi kujisahau kama wanataka kurudisha taji la Ligi Kuu Jangwani, hasa kwa kutofuatilia viporo vya Simba bali wakomalie mechi zao ili wapate matokeo mazuri ya kuwabeba.

Dk Mshindo Msolla alisema kwa jinsi ilivyo ratiba imekaa vibaya na Bodi ya Ligi inatakiwa kuliangalia hilo ili mashindano ya kimataifa yasiweze kuathiri ratiba ya michuano ya ndani kwani Simba ina viporo vingi, japo walikuwa na nafasi ya kuvipunguza kutokana na ratiba ya mashindano ya kimataifa inavyokwenda.

“Simba walivyopata ushindi wao wa kwanza nyumbani kwenye mechi ya kimataifa imepumzika wiki nzima bila kupunguza viporo, hii ratiba ni mbovu sana tofauti na wenzetu ambapo licha ya klabu kuwakilisha nchi, lakini bado haiathiri ratiba kama ilivyo kwetu,” alisema Dk. Msolla, aliyedai pengo la tofauti ya alama 20 linaweza kuwasumbua Msimbazi.

Naye nyota wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Zamoyoni Mogela alisema Simba bado ina nafasi ya kutetea ubingwa wao kama watajipangilia vizuri na kutumia vizuri kikosi chao kipana kwa kuhakikisha wanashinda michezo iliyo mbele yao hasa ya viporo.