Mechi tatu za kuibeba Pamba hizi

Wednesday February 12 2020

KOCHA Mkuu wa Pamba FC, Salvatory Edward ,Ligi Daraja la Kwanza ,Mawenzi Market , Sahare All Stars,African Lyon,Geita Gold

 

By Saddan Sadick,Mwanza

KOCHA Mkuu wa Pamba FC, Salvatory Edward amesema licha ya timu hiyo kuwa na matokeo yasiyoridhisha, atapambana kushinda mechi tatu za nyumbani kuinasua mkiani kisha kuanza harakati mpya ya kusaka nafasi nzuri.

Hadi sasa Pamba inaburuza mkia kwa pointi 13 katika Ligi Daraja la Kwanza kundi B, ambapo itakuwa na mechi tatu nyumbani ikianza dhidi ya Gipco (Jumamosi), Mawenzi Market na Sahare All Star.

Salvatory ambaye amekabidhiwa majukumu hivi karibuni ana kazi nzito ya kuinusuru timu hiyo kongwe nchini na janga la kushuka daraja.

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha huyo alisema timu ameikuta katika hali mbaya, hivyo ataanza kupambana kushinda mechi tatu za nyumbani ili kuinasua mkiani kisha kuanza hesabu upya.

Alisema kwa umoja na mshikamano baina ya uongozi, mashabiki, pamoja na wadau wa soka jijini Mwanza anaamini timu itabadilika na kumaliza ligi hiyo katika nafasi nzuri.

“Mpira ndivyo ulivyo, kimsingi ni kushirikiana katika mechi tatu za nyumbani ili kuhakikisha haturuhusu hata sare kujinasua mkiani kisha kuanza hesabu upya za namna ya kumaliza ligi,” alisema mchezaji huyo wa zamani wa Yanga.

Advertisement

Kocha huyo wa zamani wa African Lyon na Geita Gold, aliongeza kuwa kwa sasa anawaandaa kisaikolojia wachezaji ili wanapokuwa uwanjani wanapambane kusaka ushindi kwa manufaa ya timu hiyo.

“Lazima kuwahamasisha wachezaji ili wasiwe na presha wawapo uwanjani kwa sababu tunachohitaji ni kuona timu inatoka huko ilipo na kupanda juu,” alisema Salvatory.

Advertisement