Mechi tano za Simba ngumu za Afrika hizi hapa

Monday March 11 2019

 

By Khatimu Naheka

Dar es Salaam. Simba itakuwa na dakika 90 ngumu na muhimu Machi 16 pale Uwanja wa Taifa ikiwakaribisha AS Vita ya DR Congo katika mchezo wa kuwania tiketi ya kutinga hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Matokeo muhimu katika mchezo huo ni Simba kuichapa Vita Club hakuna lingine na jeuri ya wekundu hao ni moja kubwa kwamba haijawahi kupoteza nyumbani msimu huu labda rekodi hiyo iharibiwe na wapinzani wao hao.

Hata hivyo rekodi inaonyesha katika mechi tano za miaka ya karibuni kuanzia miaka ya 90 Simba imekuwa na kiburi cha kuweza kufanya kweli lakini pia ikipotea kwa nyakati zingine katika mechi za maamuzi kama hiziikifanya hivyo katika mechi mbili tofauti.

Simba vs Stella Abidjan-1993

Simba ilikutana na Stella Adjamé ya Ivory Coast katika mchezo wa fainali wa Kombe la CAF lilivyokuwa linajulikana wakati huo.

Ikianzia ugenini Simba iliilazimisha Stella suluhu kisha timu hizo kuja kumalizia mechi pale Uwanja wa Uhuru ambapo katika mshangao mkubwa wekundu hao wakapoteza kwa mabao 2-0 mabao yakifungwa na mshambuliaji Kouame Desire na Jean Ball ‘Bolizozo’.

Kabla ya mechi hizo mbili za fainali Simba iliwatoa Atletico Sport Aviacao ya Angola ikiwachapa nyumbani 3-1 kisha kuilazimisha suluhu ugenini huku Stella ikiwachapa Insuarance FC ya Ethiopia ikishinda nyumbani 3-0 kisha kuchapwa ugenini bao 1-0.

Simba vs Ismailia -2001

Simba ilijikuta inapishana na hatua ya robo fainali wakati ilipokutana na Ismailia ya Misri katika mechi ambayo iliyolazimika kuchezwa kwa siku mbili na kuwa na matokeo tofauti.

Baada ya Simba kuchapwa mabao 2-0 ugenini mchezo wa marudiano ulipigwa pale Uwanja wa Uhuru, mpaka inafika dakika ya 46 Simba ilikuwa inaongoza kwa mabao 2-0 yakifungwa na mshambuliaji Joseph Kaniki 'Golota'.

Hata hivyo mchezo huo ulilazimika kuahirishwa baada ya mvua kubwa kunyesha na kujaza maji uwanjani na kuamuliwa isitishwe kutokana na hali hiyo ya hewa na kama mechi hiyo ingeendelea maana yake ni kwamba Simba ilikuwa inahitaji bao moja pekee kusonga mbele kutokana na mabao yale mawili yalikuwa na maana Simba ilikuwa imeshasawazisha na kuwa 2-2.

Kama ingekuwa ni miaka ya sasa Simba isingekuwa na hasara hiyo kutokana na mechi ya pili ingechezwa kwa dakika zilizosalia kulingana na mechi ya kwanza iliovyositishwa huku matokeo ya mechi ya kwanza yakiendelea kama yalivyokuwa.

Mchezo huo ulirudiwa kesho yake na Simba kushinda kwa bao 1-0, lakini hata hivyo mechi hiyo iligubikwa na matukio mawili ambapo tukio la kwanza lilikuwa ni la mwamuzi kuvamiwa na wachezaji wa Ismailia kufuatia maamuzi ya kuwapa Simba penalti ambayo ingewafanya Simba kupata bao la pili na kufanya matokeo kuwa 2-0.

Baada ya mvutano huo polisi walidaiwa kuingia uwanjani kutuliza mzozo huo ambapo wakati mvutano ukiendelea inadaiwa mchezaji wa Ismailia, Emad El Nahhas alishambuliwa na kitu kama chupa iliyovunjika na kumpa jeraha kubwa na shabiki mmoja na mechi kuishia njiani na Simba kung'olewa kwa jumla ya mabao 2-1.

Simba vs Zamalek-2003

Simba ilifanya kweli tena kibabe mwaka 2003 baada ya kucheza kiume na kuing'oa Zamalek ya Misri katika mchezo wa ugenini ambao uliwapa ushujaa mkubwa.

Ikianzia nyumbani Simba chini ya kocha Mkenya marehemu James Siang'a ilifanikiwa kuichapa Zamalek kwa bao 1-0, lakini walipoenda ugenini nao wakapata kipigo kama hicho na kuifanya mechi hiyo kumalizika kwa sare ya 1-1.

Mechi hiyo iliifanya kwenda katika hatua ya mikwaju ya penalti na Simba kushinda kwa jumla penalti 3-2 matokeo yaliyowafanya kutinga hatua ya makundi.

Hata hivyo Simba haikufanya vizuri katika hatua ya makundi ikishinda mbili kupoteza tatu na sare moja ikimaliza nafasi ya tatu wakiwa na pointi saba na kuwafanya vinara Enyimba ya Nigeria na Ismailia zikitinga hatua inayofuata ambapo baadaye timu hizo kufanikiwa kufuzu nusu fainali na zote kukutana fainali na Enyimba kuwa bingwa.

Simba vs Wydad Casablanca- 2011

Mwaka 2011 Simba ilikutana na bahati baada ya awali kukutana na TP Mazembe na kuchapwa lakini baadaye Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuing'oa Mazembe kupitia rufaa waliyokatiwa na Esperance ya Tunisia.

Ilikuwa hivi baada ya Simba kuing'oa Elan Club ya Comoro kwa jumla ya mabao 4-2 katika hatua ya awali wa Ligi ya Mabingwa, wekundu hao wakakutana na TP Mazembe ya DR Congo katika raundi ya kwanza.

Mazembe ilifanikiwa kushinda mechi zote mbili ikitangulia kushinda nyumbani kwa mabao 3-1 kisha kupata ushindi mwingine pale Uwanja wa Taifa jijini Dar kwa mabao 3-2.

Wakati Mazembe ikifuzu hatua ya pili ikakutana na Wydad ambapo Wydad alifanikiwa kushinda nyumbani kwa bao 1-0 kisha ugenini wakapoteza kwa mabao 2-0.

Ikijua imefuzu hatua inafuata Caf iliwashushia rungu Mazembe wakiwaondoa kwenye mashindano kufuatia klabu hiyo kukatiwa rufaa katika kumsajilli beki wao wao Janvier Bokungu ambapo shirikisho hilo liliamua Wydad kukutana na Simba iliyong'olewa na Mazembe awali kukutana katika uwanja huru.

Hata hivyo Simba katika mechi hiyo ilijikuta ikipoteza kwa mabao 3-0 ikipoteza nafasi ya kutinga hatua ya makundi na kudondokea kombe la Shirikisho ambako nako ikatua kwa DC Motema Pembe na Simba kushinda nyumbani kwa bao 1-0 kisha ugenini kukubali kipigo cha mabao 2-0 na kukosa tena nafasi ya kutinga hatua ya makundi ya kombe la Shirikisho.

Simba vs Nkana 2018

Simba ilifuzu katika mechi nyingine ngumu ya kuamua anaenda au anabaki bada ya kuwaondoa Nkana FC ya Zambia katika Ligi ya Mabingwa ikipoteza ugenini na kushinda nyumbani.

Ikianzia ugenini Simba ilikubali kichapo cha mabao 2-1 kwa mabao mawili ya Ronald Kampamba na Kelvin Kapamba huku bao muhimu na pekee la ugenini kwa Simba likifungwa kwa penalti na nahodha wake John Bocco.

Katika mechi ya marudiano licha ya Nkana kutangulia kupata bao la kuongoza kupitia kwa nahodha wake Walter Bwallya, Simba ilipindua matokeo kwa kusawazisha kisha kupata mabao ya ushindi kupitia mabao ya viungo Jonas Mkude na Clatous Chama na mshambulaiji Meddie Kagere na kuifanya  timu hiyo kufuzu hatua ya makudi kwa jumla ya mabao 4-3.

 

 

Advertisement