Mechi tano za Man United v Liverpool hatari tupu!

Muktasari:

Kipute kitapigwa huko Old Trafford, uwanja ambao Liverpool hajawahi kushinda kwenye ligi tangu Machi 2014. Hiyo kesho patachimbika.

MANCHESTER United na Liverpool ngoma droo. Hivyo ndivyo yanavyosomeka matokeo yao kwenye mechi tano zilizopita walipokutana kwenye Ligi Kuu England. Kwenye mechi hizo, Man United imeshinda moja na Liverpool moja, huku kukiwa na sare tatu. Man United alishinda msimu uliopita kwenye mechi ya raundi ya pili, wakati Liverpool imeshinda msimu huu kwenye raundi ya kwanza. Sasa, kesho Jumapili vigogo hao wenye upinzani mkali watamalizana kwa kucheza mechi yao ya pili kwenye ligi msimu huu. Kipute kitapigwa huko Old Trafford, uwanja ambao Liverpool hajawahi kushinda kwenye ligi tangu Machi 2014. Hiyo kesho patachimbika. Mechi hiyo ya marudiano, Liverpool itakwenda kuikabili Man United yenye kocha mpya kabisa, si yule iliyempiga 3-1 kwenye mechi ya kwanza, Jose Mourinho.

Mchezo huo wa kesho unatazamiwa kuwa na mvuto wa kipekee hasa ukizingatia Kocha wa Man United, Ole Gunnar Solskjaer ni mfuasi wa soka la kushambulia tofauti na mtangulizi wake, Mourinho aliyejipatia umaarufu kwa kupaki basi. Jurgen Klopp anayehitaji kupata matokeo pia ili akimbizane vyema na Manchester City kwenye mbio za ubingwa, huku Ole akitaka matokeo ya kumfanya abaki ndani ya Top Four.

Mechi nyingine ya ligi itakayopigwa kesho, Arsenal itakuwa nyumbani Emirates kuikaribisha Southampton.

Hiyo kesho, mashabiki wakishamalizana na mambo ya Old Trafford, watasubiri kuona kile ambacho pengine mashabiki wa Chelsea watakuwa hawakipendi zaidi kije kwa wakati huu. Hii inaitwa usiyempenda kaja. Kocha Maurizio Sarri, akiwa hata hajasahau zile 6-0 alizopigwa kwenye ligi, ghafla tu, wabaya wake Man City hao wamekuja tena.

Safari hii vita yao itakuwa kwenye fainali ya Kombe la Ligi, mechi inayodaiwa Chelsea akifungwa tena tu, basi Sarri huenda akafungashiwa virago vyake na kuambiwa kwaheri.

Ni mechi ngumu na hakika hakutakuwa na kitu chepesi katika mchezo huo, Sarri akitaka kulinda ajira yake na mastaa wake wakitaka kuwaondoa aibu mashabiki wao kwa kupiga zile Sita Bila kwenye mechi iliyopita walipokutana na chama hilo la Pep Guardiola.

Kuhusu ligi, mechi nyingine zitakazopigwa leo Jumamosi ni pamoja na Tottenham Hotspur itakayokuwa ugenini kwa Burnley, huku Bournemouth ikiwa mwenyeji wa Wolves na Newcastle United ikicheza na Huddersfield kabla ya Leicester City kujimwaga King Power kumkabili Wilfried Zaha na chama lake la Crystal Palace.