Mechi 10 zilizokula kichwa cha Zahera

Muktasari:

Mwanaspoti linakuletea orodha ya mechi 10 ambazo pengine zimechangia kwa kiasi kikubwa uamuzi wa kutimuliwa kwa Zahera kutokana na kiwango duni ambacho Yanga ilikionyesha huku ikishindwa kupata matokeo yaliyotarajiwa.

Uongozi wa Yanga umeamua kuachana na Kocha Mwinyi Zahera kutokana na sababu mbalimbali.

Usajili usioridhisha ambao kocha huyo aliupendekeza kabla ya kuanza kwa msimu huu, kiwango kisichovutia cha timu, kikosi kutokuwa na muunganiko mzuri hadi sasa pamoja na matokeo yasiyoridhisha.

Matokeo ya kufungwa nyumbani na ugenini na timu ya Pyramids FC kutoka Misri katika hatua ya mchujo ya Kombe la Shirikisho kunaonekana kama sababu iliyochochea kutimuliwa kwa Zahera lakini kabla hata hawajakutana na timu hiyo, maisha ya kocha huyo ndani ya Yanga yalikuwa shakani.

Imani ya Wanayanga kwa Zahera ilianza kupungua kabla hata ya mechi hiyo kutokana na timu hiyo kutoonyesha kiwango bora katika idadi kubwa ya michezo huku ikipoteza baadhi ya mechi hizo.

Mwanaspoti linakuletea orodha ya mechi 10 ambazo pengine zimechangia kwa kiasi kikubwa uamuzi wa kutimuliwa kwa Zahera kutokana na kiwango duni ambacho Yanga ilikionyesha huku ikishindwa kupata matokeo yaliyotarajiwa.

1. Yanga 3-3 Polisi Tanzania
Ikiwa imeshapoteza mchezo wa kwanza wa ligi dhidi ya Ruvu Shooting, Yanga iliingia kwenye mchezo huo wa pili dhidi ya Maafande wengine, ikiwa na matumaini ya kupata ushindi wa kwanza ili kupooza machungu ya mechi ya ufunguzi.

Hata hivyo, mambo yalikuwa tofauti kwani badala ya ushindi, ililazimika kutoka nyuma na kusawazisha baada ya kutanguliwa kufungwa mabao 3-1 na Polisi Tanzania ambayo ilionyesha soka safi ndani ya uwanja, ikimiliki mpira karibu katika muda wote wa mchezo na ilikuwa ni kama muujiza tu kwa Yanga kusawazisha mabao hayo licha ya kwanza ilikuwa uwanja wa nyumbani.

2. Ruvu Shooting 1-0 Yanga
Baada ya kutumia zaidi ya Shilingi 1 bilioni kusuka kikosi chake kwa ajili ya msimu huu, Yanga iliingia kwenye mchezo wa ufunguzi wa ligi dhidi ya Ruvu Shooting ikiwa na matumaini makubwa ya kupata ushindi mnono.

Hata hivyo, mambo yalikuwa tofauti kwao kwani ilijikuta ikilala kwa bao 1-0 huku ikizidiwa kwa kiasi kikubwa na wapinzani wao ambao thamani ya kikosi chao hakifikii hata robo ya kile cha Yanga.

3. Yanga 1-1 Kariobangi Sharks
Baada ya kugawa vipigo dhidi ya timu dhaifu za madaraja ya chini katika mechi za maandalizi ya msimu mpya, Yanga iliialika Kariobang Sharks ya Kenya ili kucheza nayo mchezo wa kirafiki wa kimataifa katika kilele cha Maadhimisho ya Tamasha lake la Wiki ya Mwananchi, Agosti 4 mwaka huu.

Hata hivyo, kilichotarajiwa na mashabiki hakikuonekana kwani Yanga ilionyesha kiwango cha chini kulinganisha na wapinzani wao na ilijikuta ikiokolewa na bao lililotokana na mkwaju wa penati ili kusawazisha bao baada ya kutanguliwa kufungwa na wageni wao.

4. Yanga 1-1 Ndanda
Hadi inakutana na Yanga Ndanda haikuwa na matokeo ya kuridhisha katika Ligi Kuu lakini katika hali ya kushangaza, ilichukua pointi moja muhimu huku ikionyesha kiwango bora jambo ambalo halikuwafurahisha wapenzi wengi wa Yanga kwani matokeo hayo yaliwapunguza kasi katika vita ya kusaka ubingwa msimu uliopita.

5. Stand 1-0 Yanga

Stand United ilikuwa imepoteza mechi tatu mfululizo za Ligi Kuu dhidi ya timu za Biashara United, Mbao na African Lyon kabla haijakutana na Yanga katika mchezo uliochezwa Januari 19 mwaka huu.

Hata hivyo, katika hali ya kushangaza ilikuja kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Yanga huku ikionyesha kiwango bora lakini katika hali ya kushangaza, Zahera alilalamikia waamuzi walichangia timu yake ifungwe.
6. Singida 0-0 Yanga

Yanga ilionyesha kiwango duni dhidi ya vibonde Singida United katika mchezo ambao ilihitajika kupata ushindi ili ijiweke pazuri kwenye vita ya ubingwa lakini ikajikuta ikilazimishwa sare ya bila kufungana.

7. Lipuli 1-0 Yanga

Baada ya kuponea chupuchupu katika mchezo wa kwanza jijini Dar es Salaam ilioshinda bao 1-0, Yanga ilijikuta kwenye wakati mgumu pale iliporudiana na Lipuli FC katika mechi ya marudiano ya Ligi Kuu ambayo ilifanyika katika uwanja wa Samora, Iringa ambao ilichapwa bao 1-0.

Kipigo hicho kiliendana na soka safi lililoonyeshwa na Lipuli huku Yanga ikionekana kukosa muunganiko mzuri ndani ya uwanja.

8. Lipuli 2-1 Yanga (FA)

Ikiwa imeshapoteza matumaini ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu, ndoto iliyobakia kwa Yanga ilikuwa ni kutwaa ubingwa wa Kombe la Azam Sports Federation ili angalau iondoke na taji kwa msimu wa 2018/2019.

Hata hivyo, ndoto zao zilizimwa na kipigo cha mabao 2-1 ambacho kiliendana na kiwango kibovu ambacho Yanga ilikionyesha jambo ambalo halikuwafurahisha wengi ndani ya klabu hiyo.

9.Yanga 2-3 Gor Mahia

Baada ya kuvuna pointi moja tu katika mechi tatu za mwanzo za hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2018, Yanga ilikuwa na nafasi ya kufufuka upya na kuweka hai matumaini yake ya kutinga hatua ya robo fainali ya mashindano hayo ikiwa ingeibuka na ushindi katika mchezo wa raundi ya nne nyumbani dhidi ya Gor Mahia. Hata hivyo ilijikuta ikipokea kichapo cha mabao 3-2 nyumbani huku wapinzani wao wakionyesha soka la kuvutia. Matokeo hayo yalichangia kwa kiasi kikubwa kuifanya Yanga ishike mkia kwenye kundi D lililokuwa pia na timu za Rayon Sports (Rwanda) na USM Alger (Algeria).

10. Biashara United 1-0 Yanga

Haikushangaza kuona Yanga ikifungwa na timu iliyopanda daraja kwani katika mchezo huo uliofanyika Mei 10 katika Uwanja wa Karumne mjini Musoma, wenyeji walionyesha kiwango bora zaidi ya Yanga ambayo kikosi chake kilijumuisha wachezaji mastaa na wanaolipwa kiasi kikubwa cha fedha.