Mechi 10 za kuipa Simba ubingwa

Muktasari:

Wakati watani zao Yanga ambao jana walibanwa mbavu na Polisi Tanzania kwa kulazimishwa sare kwa mara ya pili mfululizo, Simba yenyewe ilichomoza na ushindi huo dhidi ya Kagera Sugar.

SIMBA jana imetakata kwenye Uwanja wa Taifa kwa kuendeleza wimbi la ushindi kwa kuichapa Kagera Sugar bao 1-0. Hiyo inamaanisha kwamba wakishinda mechi zingine 10, wameitoa Yanga kwenye mbio za ubingwa.

Hizo ni hesabu za haraka haraka baada ya kufikisha pointi 59 jana na kujikita kileleni mwa Ligi Kuu Bara. Azam inafuatia kwenye msimamo huo ikiwa na pointi 44 na Namungo pointi 40 huku Yanga ikiwa ya tatu na pointi zao 40.

Iko hivi, Simba walio chini ya tajiri mkubwa Afrika, Mohammed Dewji, kama watashinda mechi hizo 10, watakuwa na jumla ya pointi 92 ambazo hazitafikiwa na timu nyingine yeyote kwenye ligi hiyo yenye klabu 20.

Mpaka sasa Azam imecheza mechi 22 na kupata pointi 44, wakishinda michezo yao 16, iliyosalia watajikusanyia jumla ya pointi 92.

Yanga ambao wanalingana pointi na Namungo, wamecheza mechi 21 na kupata pointi 40, katika michezo yao 17 iliyobaki, hata wakishinda yote, watapata pointi 91.

Hivyo, katika hilo Yanga, Azam na Namungo watakuwa na kazi ya kuwaombea mabaya Simba ambao wako kwenye mbio za kutetea ubingwa huo kwa mara ya tatu mfululizo.

Wakati watani zao Yanga ambao jana walibanwa mbavu na Polisi Tanzania kwa kulazimishwa sare kwa mara ya pili mfululizo, Simba yenyewe ilichomoza na ushindi huo dhidi ya Kagera Sugar.

Yanga ambayo ndio inaonekana kuwa mshindani wa karibu wa Simba, ililazimishwa sare ya bao 1-1 na Polisi Tanzania ikiwa imetoka kutoka sare ya bila kufungana na Tanzania Prison kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Lakini, Simba yenyewe imezidi kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi huku ikivunja mwiko wa kushindwa kupata matokeo mbele ya Kagera Sugar tangu mwaka 2016 kwenye ardhi ya jiji la Dar es Salaam.

Katika mchezo huo wa jana uliopigwa Uwanja wa Taifa, Simba walianza kwa kasi na dakika ya 13, Meddie Kagere alifanya jaribio kwa shuti kali ambali liliokolewa na kipa wa Kagera Sugar, Benedict Tinoco huku shuti lingine la dakika 35 la Jonas Mkude likigonga mwamba.

Katika kipindi chote, Simba ambayo jana ilikamilika idara zote, ilicheza soka la kuvutia na la kasi na kuwafanya mashabiki wake kushangilia mwanzo mwisho.

Kagere akicheza sambamba na pacha wake, John Bocco wakisaidiwa kusukuma mashambulizi na viungo Francis Kahata na winga Luis Miquissone na Cloutos Chama waliliandama kwa fujo lango la Kagera.

Hata hivyo, kama sio uimara wa nahodha wa Kagera Sugar, Juma Nyosso basi mambo yangekuwa mabaya zaidi kwa Wakata Miwa hao wa Kagera.

Dakika chache kabla ya mapumziko, Chama nusura awainue mashabiki baada ya kugongeana vyema lakini, walinzi wa Kagera walikuwa makini kuondosha hatari.

Kipindi cha pili, Simba walirudi kwa kasi na kuendeleza mashambuzi langoni mwa Kagera Sugar na dakika ya 60, Bocco aliingia na mpira kwa kasi ndani ya eneo la hatari la Kagera na kufanyiwa madhambi na Tinoco na mwamuzi kuamuru upigwe mkwaju wa penati uliokwamishwa wavuni na Kagere akiongeza bao na kufikisha 13 kwenye akaunti yake.

Kabla ya mchezo huo, Simba iliingia uwanjani ikiwa imevuna alama 12 katika michezo mitano waliyocheza mwezi huu, na kuzidiwa alama moja na Ndanda FC ambayo leo Jumatano itakuwa nyumbani kuikaribisha Azam FC.

Vinara hao wa Ligi Kuu katika mchezo mitano iliyopita kabla mchezo na Kagera ilikuwa imeshinda minne na kuchapwa mchezo mmoja dhidi ya JKT Tanzania kwa kukubali kulala kwa bao 1-0 katika Uwanja wa Uhuru, Februari 7.

Tangu kocha wa Kagera, Mecky Mexime alipokabidhiwa kikosi hicho msimu wa mwaka 2017/18 amekutana na Simba kwenye Ligi Kuu katika michezo sita na kushinda mitatu pekee.

Msimu wake wa kwanza ndani ya Kagera akiwa anatoka kitoka Mtibwa Sugar, Mexime aliiharibu rekodi ya Simba iliyokuwa imecheza michezo 27 bila kupoteza kwa kuichapa bao 1-0 lililofungwa na Christopher Edward.

Kagera iliinga katika mchezo wa jana ikiwa imecheza michezo mitano nyumbani na kushinda michezo mitatu kwa kuichapa Singida United 3-0, ikaja kuifungashia virago Mwadui FC kwa kuifunga 2-1 na ikavuna alama tatu kwa Mbao FC kwa ushindi wa mabao 2-0.

Katika michezo hiyo mitano imekubali kichapo kimoja kwa kulala 2-1 dhidi ya Alliance huku ikiambulia moja walipobanwa mbavu na Biashara United walipotoka suluhu na kufanya iwe imevuna alama 10 katika michezo hiyo mitano.

Simba: Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Luis Miquissone, Clatous Chama, John Bocco, Maddie Kagere na Francis Kahata.

Kagera Sugar: Benedict Tinoco, Ally Shomary, David Luhende, Erick Kyaruzi, Juma Nyosso, Zawad Mauya, Yusuph Mhilu, Abdallah Seseme, Kelvin Sabato, Nassoro Kapama na Ally Ramadhan.