Mdamu aitikisa Simba, Chama ajibu mapigo

Muktasari:

Mdamu ni kama ameshaizoea kuifunga Simba kwani hilo ni bao lake la pili anaifunga timu hiyo, bao lingine aliwafunga Oktoba 30  mwaka jana kwenye  mchezo wa Ligi Kuu Bara msimu huu uliofanyika Uwanja wa Kambarage Shinyanga.

SIMBA na Mwadui zimeenda mapumziko zikitoshana nguvu kwa sare ya bao 1-1 katika mchezo wa Kombe la Shirikisho (FA) unaochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mabao ya Gerlad Mdamu wa Mwadui dakika  ya 35  na Clatous Chama dakika ya 45 yalizipeleka timu hizo mapumziko zikiwa sawa.
Mdamu ni kama ameshaizoea kuifunga Simba kwani hilo ni bao lake la pili anaifunga timu hiyo, bao lingine aliwafunga Oktoba 30  mwaka jana kwenye  mchezo wa Ligi Kuu Bara msimu huu uliofanyika Uwanja wa Kambarage Shinyanga.
Kabla ya mchezo huo jana, Mdamu aliliambia gazeti la Mwananchi kuwa lazima aifunge Simba leo kwani hakuna beki katika kikosi chao anayemuhofia.
Kauli yake hiyo imetimia baada ya kuifunga Simba kwa bao safi, akiachia shuti kali akimalizia krosi ya Ludovic Evance.
Kuingia kwa bao hilo ni kama kuliwaamsha Simba ambayo ilichangamka na kusaka bao la kusawazisha na  kufanikiwa kupitia kupita Chama ambaye aliwapiga chenga wachezaji watatu wa Mwadui na kuachia shuti kali  lililotinga wavuni.
Katika mchezo huu Simba imeonekana kucheza taratibu huku Mwadui ikionyesha utulivu mkubwa katika safu yake ya ulinzi.
Safi ya ulinzi ya Mwadui inayoongozwa na mchezaji wa zamani wa Simba, Joram Mgeveke, Agustino Simon, Khalfan Mbaruku, Mfaume Omary na Enrick Nkosi imeonekana kivutio kutokana na kucheza kwa nidhamu dakika nyingi za mchezo.
Mabeki hao, Mwadui inapokuwa na mpira baadhi wanapanda kushambulia na Simba inapokuwa na mpira wanarudi wote nyuma haraka kwenda kukaba wakisaidiwa na safi yao ya kiungo.