Mdachi wa Chelsea asema Hazard auzwe tu

Muktasari:

Mkataba wa Hazard utafika tamati mwishoni mwa msimu ujao na kocha Maurizio Sarri ameshamwambia wazi bilionea mmiliki wa klabu hiyo Roman Abramovich kwamba itakuwa jambo gumu sana kuendelea kubaki na staa huyo kwenye kikosi chao.

STAA wa zamani wa Chelsea, Jimmy Floyd Hasselbaink amewaambia mabosi wa timu hiyo walimpige tu bei Eden Hazard kama kutakuwa na mkwanja wa Pauni 100 milioni mezani.

Mdachi huyo aliyefunga mabao 88 katika mechi 177 alizochezea Chelsea, amewataka mabosi wa timu hiyo ya Stamford Bridge kumpiga chini Mateo Kovacic na kisha kumrudisha Alvaro Morata kwenye kikosi.

Hazard amekuwa akihusishwa na mpango wa kwenda kujiunga na Real Madrid inayonolewa na Mfaransa Zinedine Zidane na Jimmy anaamini kwamba hakuna haja ya kuendelea kumng’ang’ania mchezaji huyo kama anataka kuondoka.

Mkataba wa Hazard utafika tamati mwishoni mwa msimu ujao na kocha Maurizio Sarri ameshamwambia wazi bilionea mmiliki wa klabu hiyo Roman Abramovich kwamba itakuwa jambo gumu sana kuendelea kubaki na staa huyo kwenye kikosi chao.

Hasselbaink alisema: “Nadhani kwa sasa mpira upo kwenye miguu ya Hazard ni yeye ndiye mwenye kuamua kuhusu hatima yake kama abaki Chelsea msimu ujao au aondoke zake.

“Chelsea wao kwa upande wao wamefanya kila walichoweza kukifanya kumtaka abaki, lakini sasa mambo magumu mwaka mmoja umebaki na hakuna makubaliano yoyote. Hazard ni wa Pauni 100 milioni na Chelsea watakuwa wendawazimu kukataa kiasi kama hicho cha pesa.”