Mdachi Kiungo mshambuliaji anayekinukisha Sauzi

Muktasari:

  • Mdachi ambaye alitembelea ofisi zetu zilizopo Tabata jijini Dar Salaam, zinazochapisha gazeti hili la Mwanaspoti, Mwananchi na The Citizen anasema amepata mialiko ya kwenda kufanya majaribio Dubai na Russia mwezi huu wa Aprili na ujao wa Mei.

KUNA kiumbe mmoja kutoka Korea Kusini anaitwa Son Heung-min, ametawala midomoni mwa wapenzi na mashabiki wa soka la Asia basi hivyo ndivyo Jafary Abdul ‘Mdachi’ wa Summerfield Dynammos ya Afrika Kusini anavyoota siku moja aiteke Afrika.

Son ambaye ni mzaliwa wa Chuncheon, Korea Kusini ni miongoni mwa mashine zinazotegemewa na kocha, Mauricio Pochettino kwenye kikosi chake cha Tottenham Hotspur ya England.

Kiwango cha nyota huyo kimewafunika wakali kibao wanaotokea Asia, akiwamo mchezaji wa zamani wa Mancheater United, Shinji Kagawa, ambaye kwa sasa anaichezea Borussia Dortmund ya Ujerumani na Aaron Mooy wa Huddersfield Town ya England.

Ndoto ya ‘Mdachi’ ambaye ni chipukizi wa Kitanzania, anayecheza soka la kulipwa Afrika Kusini ni kujipatia mafanikio na heshima kama Son ambaye aliwahi kuwa mfungaji bora wa Kombe la FA England msimu wa 2016/17.

Mdachi ambaye alitembelea ofisi zetu zilizopo Tabata jijini Dar Salaam, zinazochapisha gazeti hili la Mwanaspoti, Mwananchi na The Citizen anasema amepata mialiko ya kwenda kufanya majaribio Dubai na Russia mwezi huu wa Aprili na ujao wa Mei.

“Nataka kuwa mchezaji mkubwa siyo nyumbani Tanzania tu ndio maana niliondoka ili kwenda kwenye taifa (Afrika Kusini) ambalo ningepata nafasi zaidi ya kuonekana.

“Nilifanya mawasiliano na wakala ambaye alinihakikisha kunisaidia kupata timu Afrika Kusini, sikuzamia kama ilivyo kwa wachezaji wengi wa Kitanzania ila changamoto kubwa ilikuwa ni kupata kibali cha kazi.

“Kibali cha kazi Afrika Kusini kina mchakato ambao unachosha kwakeli, lakini ulipokamilika ilibidi timu yangu itume kwanza taarifa zangu kwa shirikisho la soka Tanzania (TFF) ili wathibitishe kabla ya kuruhusiwa kuanza kucheza,” anasema Mdachi.

Baada ya taarifa zake kuifikia TFF na kurudishwa Afrika Kusini msimu ulikuwa umeshamalizika hivyo hakupata nafasi ya kucheza mechi hata mmoja kwenye Ligi Daraja la Pili.

Mdachi anasema maisha yaliendelea na taratibu akaizoea Afrika Kusini na hatimaye akaibukia G.W.P Friends kwa mkopo.

“Nimecheza karibu msimu mzima ila imebidi nirejee nyumbani mara moja kwa ruhusa maalumu ili nifanikishe suala langu la taratibu za safari ya kwenda kufanya majaribio.

“Nina nafasi mbili za kwenda kufanya majaribio ya kwanza ni Aprili 15 nchini Russia ya pili ni Dubai, kuna wakala anaitwa Aliu Rahman huyo ndo kuna timu ameongea nazo Ulaya.

“Naamini kuwa nina kipaji cha kucheza Ulaya na hii ni nafasi ambayo naamini itakuwa kama upenyo wa kuendelea kupigania ndoto zangu.

“Dubai kwenyewe kuna ndugu yangu ambaye amenifanyia mpango wa kwenda timu moja hivi inaitwa Al Wahda,” anasema.

Mdachi mwenye umri wa miaka 18 ni mtoto wa nyota wa zamani wa Yanga, Maneno Abdul, ambaye aliichezea timu hiyo ya wanachi kwa mafanikio makubwa kabla ya kutimkia zake Dubai ambako alienda kumalizia soka lake.

Kinda huyo anasema amekuwa na mahusiano mazuri na nyota wengine wa Kitanzania wanaocheza soka la kulipwa Afrika Kusini, akiwamo Uhuru Seleman wa Royal Eagles ya Daraja la Kwanza nchini humo.

“Huwa tunaishi vizuri Watanzania ambao tupo kule. Licha ya kwamba kila mmoja anapambana kwa upande wake, lakini huwa tunakumbukana na kusalimiana kwa sababu safari yetu ni moja,” anasema.

“Nchi za wenzetu kila mtu yuko bize na mambo yake unaweza kuhisi kutengwa, lakini sisi Wabongo kule Sauzi tuko pamoja,” anasema. Aidha, Mdachi anawataka nyota wenzake wa Kitanzania kutokuwa waoga wa kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.