Mchumba wa Kakolanya hataki kubaki nyuma

Muktasari:

Hadra anasema kwa sasa amerejesha majeshi Simba ambako mume wake ataanza majukumu mapya msimu ujao baada ya kuachana na Yanga, akidai atamuunga mkono mwanzo mwisho kuhakikisha anakuwa na mafanikio na kumuonyesha ushindani wa juu.

MCHUMBA wa kipa mpya wa Simba, Beno Kakolanya, anayejulikana kwa jina la Hadra ameweka wazi kwamba timu yoyote ambayo mchumba wake ataitumikia ndiyo atakayokuwa anaishangilia kwa madai kwamba kwa sasa hana timu maalumu kama zamani.
Hadra anasema kabla ya kujiingiza kwenye uhusiano na Kakolanya alikuwa anaishangilia Simba, ila baada ya kuwa chini ya kipa huyo wakati anafanya kazi Yanga basi aliamua kuweka ushabiki pembeni na kuunga mkono juhudi ya kazi ya mpenzi wake.
Hadra anasema kwa sasa amerejesha majeshi Simba ambako mume wake ataanza majukumu mapya msimu ujao baada ya kuachana na Yanga, akidai atamuunga mkono mwanzo mwisho kuhakikisha anakuwa na mafanikio na kumuonyesha ushindani wa juu.
"Popote ambapo Kakolanya atatua mimi nipo, siwezi kuacha kumuunga mkono maana ndio kazi inayofanya anitunze na maisha yetu yaendelee mbele, nimefurahi kuona amepata timu baada ya kukaa nje kwa muda mrefu.
"Naendelea kumsisitiza kwamba anaenda kwenye changamoto mpya lazima ajipange, ajitume kwa bidii katika mazoezi yake binafsi licha ya kwamba hata wakati yupo nje alikuwa anafanya programu zake.
"Namuamini mume wangu ni kipa mzuri, ataenda kuonyesha ushindani dhidi ya Aishi Manula ambaye ndiye anaonekana kuwa kipa namba moja Simba, namtia moyo ataweza na nipo bega kwa bega na yeye kuhakikisha kazi yake inakuwa ya kiwango na mvuto kwa ndani na nje ya nchi"anasema.