Mchawi wa Liverpool vs Manchester United huyu hapa

Muktasari:

  • Manchester City na Manchester United katika Uwanja wa Etihad. Katika pambano hilo ambalo City ilikuwa inahitaji kushinda kutangaza ubingwa, United ilipambana na kushinda mabao 3-2 licha ya City kuongoza 2-0 mpaka wakati wa mapumziko.

LIVERPOOL,ENGLAND.JUZI Liverpool imepita katika kundi lake la Ligi ya Mabingwa, jana Jumatano Manchester United imekamilisha ratiba yake baada ya kupita katika kundi lake, na sasa macho yake yote yameelekezwa katika pambano la Jumapili Ligi Kuu ya England. Joto limepanda.

Martin Atkinson amethibitishwa Pilato wa pambano hilo litakalopigwa Anfield Jumapili mchana huku kila timu ikiwa na umuhimu na mechi hiyo ambayo inasubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka duniani.

Atkinson alikuwa mwamuzi wa pambano la timu hizo msimu uliopita Anfield wakati timu hizo zilipotoka sare huku Kocha wa United, Jose Mourinho alishutumiwa kulipoozesha pambano hilo kwa kucheza staili ya kujihami iliyopitiliza.

Mwamuzi huyo mzaliwa wa West-Yorkshire vilevile ndiye aliyechezesha pambano baina ya timu hizo mwaka 2015. Pambano hilo linakumbukwa kwa bao murua la Juan Mata wa United lakini pia Atkinson alimtoa nje kiungo staa wa Liverpool, Steven Gerrard sekunde 38 tu baada ya kuingia uwanjani.

Aprili mwaka huu mwamuzi huyo alichezesha pambano la marudiano kati ya watani wa jadi wa Jiji la Manchester, Manchester City na Manchester United katika Uwanja wa Etihad. Katika pambano hilo ambalo City ilikuwa inahitaji kushinda kutangaza ubingwa, United ilipambana na kushinda mabao 3-2 licha ya City kuongoza 2-0 mpaka wakati wa mapumziko.

Mpaka sasa Atkinson amechezesha mechi 14 za Ligi Kuu ya England msimu huu huku akiwa ametoa kadi za njano 44 na kadi moja nyekundu kwa beki wa Brighton, Shane Duffy katika pambano dhidi ya Crystal Palace baada ya kumpiga kichwa beki wa Kidachi, Patrick van Aanholt.

Pambano la Jumapili ni mtihani mkubwa kwa timu zote mbili. Liverpool inaongoza katika ligi ikiwa na pointi 42 tofauti ya pointi moja kwa Manchester City baada ya kufungwa dhidi ya Chelsea Stamford Bridge.

Liverpool italazimisha kushinda pambano hilo kwa ajili ya kubakia kileleni mwa msimamo huku ikiombea City inayocheza dhidi ya Everton Etihad iendelee kuyumba kama ilivyotokea katika pambano dhidi ya Chelsea. Wababe hao wa Anfield pia watakuwa wakiendelea kusaka rekodi ya Arsenal ya kucheza msimu mzima bila ya kufungwa 2003/04 ambapo mpaka sasa haijapoteza pambano lolote huku City ambao ilikuwa nayo sambamba katika kuisaka rekodi hiyo ikipoteza. Mtihani mgumu utakuwa kwa Man United ambayo inalazimika kushinda katika pambano la Jumapili kwa ajili ya kujiweka karibu na nafasi nne za juu. Mpaka sasa United imeachwa pointi nane na Chelsea inayoshika nafasi ya nne katika msimamo.

United pia imeachwa pointi 16 na Liverpool na ni wazi matumaini ya ubingwa katika msimu wa tatu wa Mourinho Old Trafford yameondoka. Endapo ikipoteza katika pambano la Jumapili itakuwa wameachwa pointi 19. Na endapo ikipoteza katika pambano hilo kisha Arsenal au Chelsea zikashinda katika mechi zao za wikiendi hii, United itakuwa imeachwa pointi 11 na timu za Top Four.