Mchawi wa Kick Boxing ni huyu

Muktasari:

Akizungumzia changamoto ya kick boxing nchini, Kaseba alisema mchezo ulikufa kutokana na fitina tu, hakuna kingine.

KAMA ulikuwa mpenzi na shabiki wa kick boxing (ngumi na mateke) nchini na umekuwa ukijiuliza ni wapi mchezo huo ulipoishia msikie, Kanda Kabongo.

Bondia huyo aliyekuwa akitamba kwenye kick boxing anakwambia tangu 2011 mambo yalikuwa hayaendi kwenye mchezo huo kiasi cha yeye kuamua kuachana nayo na kuingia kwenye ngumi (boxing).

“Mfumo wa kick boxing ulibadilika, wakati Kaseba (Japhet) akiongoza mchezo huo ulikuwa na promosheni kama ilivyo kwa boxing, alianzisha hadi chama na kuchukua jukumu la kuendeleza mchezo huu.

“Tulikuwa na Ligi ya Kick Boxing ambayo ilikuwa na ushindani mkubwa tu, lakini uovu wa mabondia wenyewe mchezo umekufa, kwani mabondia wengi walijiondoa kushiriki na kutoa sababu ya kutoshiriki ligi ile kitendo ambacho kilimkatisha tamaa Kaseba,” alisema.

Anasema kwa Tanzania, Kaseba ndiye mfalme wa mchezo huo na alipojitoa kuandaa, mchezo ndiyo ukaishia hapo.

“Binafsi nilipoona mambo kwenye kick boxing hayako sawa wakati bado nina nguvu na uwezo, niliamua kuachana nazo na kugeukia kwenye ngumi mpaka sasa,” alisema Kanda Kabongo.

Akizungumzia changamoto ya kick boxing nchini, Kaseba alisema mchezo ulikufa kutokana na fitina tu, hakuna kingine.

“Tatizo lilikuwa kwa mabondia wa kick boxing baadhi kutojitambua, pamoja na kwamba nilikuwa natumia fedha yangu ya mfukoni yakaibuka majungu na fitina hadi mchezo umefika hapo ulipo,” alisema.

Alisema licha ya changamoto hiyo anafikiria kuufufua upya kwani yeye ndiye muasisi wa kick boxing nchini na tayari mchakato wa kuufufua upya umeanza.

“Kuna timu kutoka Pakistani watakuja nchini Julai kuangalia uwezekano tuwe tunashirikiana, hivyo kama mambo yakienda vizuri tutaifufua kick boxing nchini upya,” alisema Kaseba.

Mchezo wa Kick Boxing ulikuwa umeanza kupata umaarufu mkubwa chini ya Kaseba ambaye alikuwa akiandaa mapambano mbalimbali na pia akipita katika vyombo vya habari kwa ajili ya kuufanyia promosheni mchezo huo ambao awali ulionekana mgeni nchini lakini kwa juhudi yake ukafanikiwa kuwaa marufu nchini kabla ya kupotea tena.