Mbwana Makatta: Ukimzingua tu anasepa

Muktasari:

Mojawapo ya mambo aliyoyaweka wazi ni juu ya msimamo wake wa kutopenda kuingiliwa kibarua chake na mabosi na kusema, akizunguliwa kwa mtindo huo huwa hana simile, anasepa. Endelea naye...!

HAKUNA ubishi unapozungumzia makocha bora wazawa nchini, jina la Mbwana Makatta haliwezi kukosekana. Unaliachaje jina lake kando wakati ndani ya misimu mitatu ameweza kuzipandisha timu mbili Ligi Kuu Bara. Kwa nini Makatta asiwe bora.

Msimu uliopita aliipandisha daraja Alliance FC ya Mwanza kisha akazinguana nao na kutimkia Polisi Tanzania iliyokuwa Ligi Daraja la Kwanza (FDL) na kwa nusu msimu huu ameipandisha timu hiyo Ligi Kuu Bara msimu ujao.

Ni kocha huyo pamoja na Fred Felix ‘Minziro’ na Hassan Banyai kwa miaka ya karibuni ndio wameonekana vinara wa kuzipandisha timu katika madaraja tofauti na Mwanaspoti imefanya mahojiano maalumu naye na kufunguka mambo kadhaa.

Mojawapo ya mambo aliyoyaweka wazi ni juu ya msimamo wake wa kutopenda kuingiliwa kibarua chake na mabosi na kusema, akizunguliwa kwa mtindo huo huwa hana simile, anasepa. Endelea naye...!

SIRI YA MAFANIKIO YAKE

Makatta aliyenyakuwa tuzo ya Kocha Bora misimu mitatu iliyopita baada ya kuinusuru Prisons isishukle daraja, anafichua siri ya mafanikio yake katika kuzivusha timu mbalimbali kuwa ni kuwapa ujasiri wachezaji wakubaliane na hali ya matokeo mabaya katika mechi zilizopita na wajitambue wanaweza kubadilisha matokeo katika mechi zilizobakia.

“Tangu naanza kazi nimeshavusha timu nne kutoka ligi ndogo hadi Ligi Kuu na siri kubwa ni kuwajenga wachezaji kisaikolojia, hivyo kwangu sio ajabu kupandisha timu kwani imekuwa kawaida sana na hii inatokana pia na misimamo yangu ya kutokutaka kuingiliwa katika majukumu ya kazi, ndio maana ukiniingilia ni bora nikuachie niondoke,” anasema.

Mbali na Alliance na Polisi Tanzania, Makatta amewahi kuipandisha pia Mji Mpwapwa na Twiga Sports.

Kocha huyo anasema katika utendaji kazi wake anapenda mipaka kuzingatiwa, kwani kama mwalimu anajua kila anachokifanya akishauriana na benchi lake la ufundi na sio kiongozi kumuingilia na kumpangia kazi za ufundi.

Amewataka makocha wenzake wa soka kutambua taaluma zao na kuzitendea haki na kutokubali kujirahisisha wala kukubali kuingiliwa majukumu yao, pia waendelee kujiongeza katika elimu za ngazi za juu ili wafike mbali na waheshimiwe nchini.

Kuhusu kushuka kwake kufundisha timu za madaraja ya chini, Makatta anasema; “Mi huwa sioni tabu kufundisha timu ya daraja lolote lile ili mradi ni kazi ya ukocha na hata ikipanda wakiniacha sijutii maana niliingia pale kwa mkataba na tutaachana kwa mkataba kuisha.”

ALLIANCE NA POLISI TANZANIA

Makatta aliyekuwa Alliance kabla ya kutua Polisi ndani ya msimu huu mmoja, alipoulizwa tofauti za klabu hizo anasema timu zote mbili anazikubali kuwa ni timu nzuri na anazojivunia kwa vile amezifundisha kwa mafanikio.

“Alliance nimejifunza mambo mengi lakini zaidi ni timu yenye malezi ya taasisi ya michezo na vijana wanacheza soka la kisasa, lakini mafanikio yao hayawezi kutokana na wachezaji wao pekee lazima waongeze nguvu kwa wachezaji wa nje.”

Kuhusu Polisi anasema ni timu nzuri yenye ushirikiano mkubwa na benchi la ufundi na uongozi hivyo akifanikiwa kupata nafasi ya kuifundisha tena Ligi Kuu atafurahi sana na hata akiachwa atafurahi pia kuongeza idadi ya timu alizopandisha kwani mkataba wao umefikia tamati.

CHANGAMOTO ZAKE

Anapoulizwa juu ya changamoto ya kufundisha timu ya Ligi Kuu na zile za madaraja ya chini, anaseme;

“Changamoto zimeundwa kwa ajili ya kufikia mafanikio endapo ukiweza kutatua hivyo changamoto za ligi daraja la kwanza ni nyingi, ila wengine wanafanikiwa kutatua na kuvuka.” Anasema klabu nyingi za FDL zipo duni havina vyanzo vya mapato, hivyo uendeshaji wake unakuwa mgumu na kuwataka TFF watafute udhamini ili ligi hiyo iwe rahisi. Anawataka wadhamini waangalie pia FDL kuwasaidia, pia Azam nao waangalie kwenye chaneli zao wasaidie zionyeshwe mubashara kupunguza baadhi ya figisu na vitendo vya kikatili katika ligi hiyo.

MAKATTA NI NANI?

Kocha huyu ni mzaliwa wa jiji la Tanga alianza kufahamika kwenye soka miaka ya 1980 alipoanza kucheza akiwa na miaka 17, akikumbuka mwaka 1984 alipoanza makeke kama kipa wa Reli Iringa na kupita klabu moja hadi nyingine hadi leo akiwa moja ya makocha hodari.

“Nilicheza klabu ya Reli Iringa ikiwa Daraja la Tatu kabla ya mwaka 1985 kuhamia Waziri Mkuu ya Dodoma kabla ya kusajiliwa Tukuyu Stars mwaka 1986 na kupanda nao Ligi Daraja la Kwanza (sasa Ligi Kuu Bara),” anasema.

“Baada ya hapo nilisajiliwa Yanga mwaka 1987 niliyotumikia hadi mwaka 1991 na kubeba nao ubingwa wa Ligi Kuu mara nne mfululizo kabla ya kuhamia Kagera mwaka 1992 na kuichezea RTC, ila nilipata majeraha ya bega na matibabu yake yalinigharimu kwa kushindwa kucheza hivyo nikaacha nijiuguze.”

SAFARI YA UKOCHA

Makatta anasema baada ya kupona majeraha ya bega hakuweza tena kucheza mpira bali alijikita katika biashara zake bianfsi.

“Nikiwa nafanya baishara zangu kama miaka mitano hivi, nilikuwa bado napenda soka na kwa sabahu siwezi tena kucheza nilijiunga na mafunzo ya awali ya ukocha mwaka 1997 na baada ya kumaliza 1998/1999 nilianza ajira yangu ya kwanza katika timu ya Mji Mpwapwa ya Dodoma nilifanikiwa kuivusha kutoka SDL hadi FDL (Ligi Kuu ya sasa).”

Anasema Mji ilizisumbua sana Simba na Yanga jambo lililofanya vigogo hao kuibomoa kwa kusajili nyota wao sita tegemeo kwa mpigo akiwamo Noel Thomas alisajiliwa Yanga, Shekhan Rashid, Sunday Frank, Joel Noel na Jumanne Tondolo wakitimkia Simba.

“Baada ya mafanikio hayo 2000 nilienda Twiga Sports ya Kinondoni inayomilikiwa na Mbunge Idd Azan na kufanikiwa kuivusha kutoka Ligi Daraja la Pili hadi Ligi Kuu nikiwa na nyota waliokuwa wanakataliwa timu kubwa kwa madai wameisha kama kipa Juma Mpongo, Wilcliff Ketto, Athuman Chama, Mussa Msengi, Dua Said, Bakar Malima, Saidi Kizota na Edibily Lunyamila.”

Timu nyingine alizofundisha ni Ashanti United, Toto Africans ya Mwanza, Tanzania Prisons, Oljoro JKT, JKT Ruvu, Friends Rangers, Kagera Sugar KMC, Alliance na sasa Polisi Tanzania.

Anasema hakuna kitu anachojivunia kama alipoiokoa Prisons msimu wa 2014-2015 ikiwa mkiani katika duru ikisaliwa na mechi tisa na kuikoa isishuke jambo lililompa Tuzo ya Kocha Bora wa Msimu.