Mbunge Mollel ataka bunge limtambue Samatta

Muktasari:

  • Mbunge wa Viti maalum Amina Mollel amelitaka bunge kutambua mchango wa mchezaji wa taifa Mbwana Samatta na kukemea wanaomwita ni raia wa Kenya.

Dodoma. Mbunge wa Viti maalum (CCM), Amina Mollel amelitaka bunge kutoa tamko la kumpongeza mshambuliaji wa kimataifa Tanzania, Mbwana Samatta kutokana na mchango wake kwa klabu ya Genk.

Mollel aliomba mwongozo wa Spika bungeni leo Jumatano Mei 22, 2019, mbunge huyo amemtaja mchezaji huyo ambaye ni nahodha wa timu ya taifa kama shujaa.

Mollel ameomba mwongozo wa Spika akisema mchango wa Mtanzania huyo unapaswa kuthaminiwa na kujaliwa hata ndani ya bunge ili kumtia moyo.

Amesema mabao aliyoifungia timu hiyo kwenye ligi ndiyo imewezesha Genk kutwaa ubingwa wa ligi ya Ubelgiji.

Hata hivyo ametaka serikali kukemea kile kinachoendelea kwenye mitandao kuwa Samatta ni raia wa Kenya akataka jambo hilo likemewe.

Spika Job Ndugai amesema serikali imesikia na kuwa jambo hilo ni muhimu hivyo serikali iangalie namna ya kumtaja shujaa huyo.