Mbrazil Da Silva apiga moja Simba yaua 4G Sauzi

Muktasari:

Katika mchezo huo wa kirafiki Bocco alifunga mabao mawili na Hassan Dilunga bao moja katika kipindi cha kwanza kabla ya Mbrazili Da Silva kuhitimisha kuwa kufunga bao la nne.

Rustenburg.  Mabao ya nahodha John Bocco na Mbrazili Wilker da Silva yametosha kuipa Simba ushindi mzuri wa mabao 4-0 dhidi ya Orbret Tvet katika mchezo wake wa kirafiki uliochezwa kwenye Uwanja wa wa Hoteli ya The Royal Marang.

Katika mchezo huo wa kirafiki Bocco alifunga mabao mawili na Hassan Dilunga bao moja katika kipindi cha kwanza kabla ya Mbrazili Da Silva kuhitimisha kuwa kufunga bao la nne.

Hilo ni bao la kwanza kwa Mbrazili huyo tangu ajiunge na Simba mwanzoni mwa mwezi huu akitokea klabu ya Bragantino ya Brazil.

Katika mchezo huo kocha wa Simba, Patrick Aussems aligawa vikosi viwili, kikosi cha kwanza kilicheza dakika 60 na cha pili dakika 30.

Katika kikosi kilichoanza Aussems amemweka Aishi Manula golini, kulia Shomari Kapombe na kushoto Gadiel Michael. Kati yupo Mbrazili na Erasto Nyoni, viungo Mdhamiru Yassin na Jonas Mkude.

Winga ya kulia Athuman Miraji na Ibrahim Ajibu wakati washambuliaji wa kati ni John Bocco na Hassan Dilunga.

Simba imepanga kucheza mechi nne katika maandalizi yao dhidi ya Platnumz Stars, Township Rollers na Orlando Pirates kabla ya kurudi Dar es Salaam.

Taarifa zaidi kutokana na mchezo huo soma magazeti ya Mwanaspoti, Mwananchi na The Citizens.