Mbio za ubingwa Ligi Kuu England si mchezo!

Muktasari:

Haitaki maneno maneno hiyo, watashuka uwanjani Anfield kuwakaribisha Chelsea, ambao pia wenyewe wanausaka usiku wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa msimu ujao.

MCHAKAMCHAKA chinja huko kwenye Ligi Kuu England. Liverpool wamejinafasi kileleni kwenye msimamo, lakini wakifahamu wazi kwamba hiyo kesho Jumapili watakuwa kwenye wakati mgumu wa kukishikilia hicho kiti walichokikalia.

Haitaki maneno maneno hiyo, watashuka uwanjani Anfield kuwakaribisha Chelsea, ambao pia wenyewe wanausaka usiku wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa msimu ujao.

Hakika hii ni wikiendi matata kabisa kwenye mbio za kuusaka ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu, ambapo Liverpool wao wakiwa na shughuli pevu ya kumkabili Eden Hazard na jeshi lake la Chelsea, wapinzani wao kwenye mbio za ubingwa, Manchester City wao watakuwa ugenini kumenyana na Crystal Palace na Wilfried Zaha. Pep Guardiola na kikosi chake cha Man City watatangulia kuingia uwanjani, kwa maana kwamba mechi yao itachezwa mapema na kama atawachapa Palace, basi atamwondosha Liverpool kwenye kilele cha msimamo wa ligi hiyo hadi hapo watakapocheza na Chelsea na kuona matokeo watakayovuna.

Chelsea wao wapo kwenye nafasi ya tatu na pointi zao 66, watahitaji kushinda ili kuendelea kubaki hapo hadi mwisho wa msimu ili kufuzu kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Chelsea inahitaji kuzikimbia Tottenham Hotspur, yenye pointi 64 na itacheza leo Jumamosi kwa kuwakabili Huddersfield na Arsenal pia yenye pointi 63, ambayo itakipiga ugenini kwa Watford Jumatatu.

Washindani wengine kwenye Top Four, Manchester United wao Itacheza leo dhidi ya West Ham United, ambapo ushindi utawafanya kufikisha pointi 64 ambazo zitawasaidia kuwaengua Arsenal kwenye msimamo, lakini hawataingia ndani ya nne na hivyo kuendelea kukabiliwa na vita kali katika kuifukuzia tiketi hiyo ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Hivyo ndivyo ulivyo upinzani wa mechi za wikiendi hii kwenye Ligi Kuu England, ambapo kwenye mbio za ubingwa kutakuwa na taswira kubwa sana licha ya kwamba Liverpool wao itakuwa imecheza mechi moja zaidi ya wapinzani wao Manchester City.