Mbio za magari za Safari Rally zimerudi upya Kenya 2020

NAIROBI, KENYA. MASHINDANO ya mbio za magari za Kenyan Safari Rally zimerudishwa kwenye mfululizo wa mashindano ya ubingwa wa dunia ya mchezo huo mwaka 2020 ikiwa ni kwa mara ya kwanza baada ya miaka 18.
Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Chama vya Mashindano ya Mbio za Magari (FIA), Jean Todt, alitangaza Ijumaa akiwa kwamba Safari WRC imerejea baada ya kupitishwa na mamlaka ya dunia ya mchezo huo wa mbio za magari.
Mashindano hayo ya Safari Rally yatafanyika kuanzia Julai 16 hadi 19 mwakani.
Rally Monte-Carlo itafungua msimu huo kama ilivyo utamaduni, wakati raundi tatu mpya za mashindano hayo zitakuwa za Rally Kenya, Rally New-Zealand na Rally Japan, ambayo ndiyo itakayofunga msimu kwenye ubingwa huo wa dunia.
Mkurugenzi wa FIA, Yves Matton alisema: “Ili kuufanya ubingwa huo kuwa wa dunia, tulihitaji kuwa na raundi kadhaa za WRC nje ya Ulaya. Nimefurahi kuona hili lilifanyika kwa Kenya na Japan kurejea kwenye kalenda ya mwaka ya mashindano ya dunia ya mbio za dunia mwakani, sambamba na New Zealand iliyochukua nafasi ya Australia.
“Kufuatia kuishirikisha Chile mwaka jana, kalenda ya 2020 imetanuka zaidi na tutakuwapo Asia na Afrika."
Kalenda ya 2020 ya mashindano hayo ya dunia itakayohusisha raundi 14 itakuwa kama hivi ifuatavyo:
1. Rally Monte-Carlo (Januari 23-26),
2.Rally Sweden (Februari 13-16),
3.Rally Mexico (Machi 12-15)
4. Rally Chile (Aprili 16-19),
5. Rally Argentina (Aprili 30-Mei 3),
6. Rally Portugal (Mei 21-24),
7. Rally Italy (Juni 4-7),
8. Safari Rally (Julai 16-19),
9. Rally Finland (Agosti 6-9),
10. Rally New Zealand (Septemba 3-6),
11. Rally Turkey (Septemba 24-27),
12. Rally Germany (Oktoba 15-18),
13. Rally Great Britain (Oktoba 29-Novemba 1),
14. Rally Japan (Novemba 19-22)