Mbinu za kuibeba Simba kimataifa

Muktasari:

Kila kukicha kumekuwa kukiibuka fitna mbalimbali katika soka. Timu moja hufanya ili kuwapunguza nguvu wapinzani wao. Hili sio jambo geni kwa Simba na Yanga ambazo zimekuwa zikishiriki mara kwa mara katika michuano ya kimataifa

KUNA mambo matatu ambayo yamekuwa yakizibeba Al Ahly, TP Mazembe na Zamalek ambao wametawala soka la Afrika katika ngazi ya klabu.

Kwanza uwezo mkubwa wa kifedha, ushindani kutoka katika ligi za ndani kwenye mataifa wanayotoka na uzoefu wa kiushindani walionao.

Miamba hiyo ya soka Afrika hakuna klabu ambayo inaweza kuiyumbisha linapokuja suala la kusajili mfano Januari mwaka huu, Al Ahly ambao ni mabingwa mara nane wa Ligi ya Mabingwa Afrika walipata saini ya Msenegal Aliou Badji kutoka Rapid Vienna ya Austria.

Klabu za ukanda wa Afrika Mashariki haziwezi kutunishiana misuli na miamba hiyo iwe kifedha, ushindani walionao na hata uzoefu, lakini kuna mambo ambayo wanaweza kufanya yakasaidia kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa mbele ya vigogo hao.

Zipo klabu zenye uwezo mkubwa kifedha zinatoka katika ligi zenye ushindani pamoja na uzoefu walionao zimekuwa zikiangukia pua katika michuano hiyo, mfano 2018, TP Mazembe walikiona cha moto kutoka kwa 1º de Agosto. Timu hiyo kutoka Angola iliing’oa TP Mazembe katika robo fainali.

Kwa Tanzania wamepatikana wawakilishi wa Ligi ya Mabingwa msimu ujao, ambao ni Simba, baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu. Haya hapa ni mambo ya msingi ambayo yanaweza kuwasaidia Simba.

 

USAJILI

Juni 9, mwaka huu, Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi ya Simba, Mohammed Dewji kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter aliandika ujumbe uliosomeka: “Wanasimba wenzangu nataka niwahakikishie hakuna mchezaji wetu yeyote atakayeondoka Simba. Lakini pia tutasajili mchezaji yoyote kutoka popote kama mwalimu wetu atamuhitaji kwenye kikosi chake. Tutashuka kwa kishindo, hatuna maneno mengi lakini tupo.”

Hakuishia hapo akahoji kwa kuuliza wafuasi wake katika ukurasa huo kuwa wangependa waanze na nani? Kwa miaka mingi Simba na Yanga wamekuwa na changamoto ya kusajili wachezaji wa kigeni ambao viwango vyao huonekana vya kawaida.

Kufanya vizuri katika mashindano makubwa kuna uhitaji wa kufanya usajili wa nguvu kulingana na mahitaji ya mwalimu na sio kufanya ilimradi usajili tu. Upungufu ambao umeonekana katika kikosi cha Simba upo katika maeneo makuu manne ambayo yanapaswa kuimarishwa.

Eneo la kwanza ni upande wa beki wa kulia, ukimuondoa Shomari Kapombe ambaye amekuwa akicheza mpira wa kisasa, anamudu kushambulia na kukaba hakuna mchezaji mwingine mwenye ubora huo. Haruna Shamte ni mzuri katika kuzuia pekee na habari za uhakika ni kwamba Simba watamtoa kwa mkopo.

Tangu kuondoka kwa James Kotei, Simba imekosa kiungo mkabaji mwenye uwezo wa kupoza mashambulizi ya wapinzani wao, ambaye angesaidiana na Jonas Mkude, badala yake wamekuwa wakicheza Mzamiru Yassin na muda mwingine Gerson Fraga waliokosa mwendelezo wa kuonyesha kiwango cha juu katika michezo mfululizo.

Simba wanahitaji kiungo mshambuliaji mwenye uwezo wa daraja kama la Clatous Chama ambaye ataongeza makali kutengeneza nafasi za mabao katika meneo ya pembeni, kwa maana ya mawinga wanaonekana kukamilika kutokana na ubora walionao Shiza Kichuya, Francis Kahata, Deo Kanda, Luis Jose Miquissone na hata Hassan Dilunga ambaye muda mwingine hutokea pembeni.

Eneo la mwisho ni katika safu ya ushambuliaji ambayo kwa sasa imekuwa ikiwategemea John Bocco na Meddie Kagere. Simba wanatakiwa kuongeza mshambuliaji mwingine wa nguvu ambaye ataleta changamoto kwa Bocco na Kagere.

Awamu iliyopita Simba walichemka kwa Wilker Henrique da Silva ambaye hakuwa lolote na mwisho wakaachana naye, hivyo ni muhimu kwao kuwa na utulivu katika kusajili vinginevyo inaweza kuwagharimu wakati wa mashindano kwa sababu kuna suala la majeraha ambalo halitabiriki.

 

KIKOSI KIPANA

Kutokana na ushiriki wao katika michuano ya kimataifa, Simba inapaswa kuwa na kikosi kipana chenye wachezaji wenye ubora wa juu ambacho kitamudu kushiriki michuano mbalimbali kwa wakati mmoja.

Kama wasipokuwa na kikosi kipana huenda nguvu ta ushindani ikaegemea upande mmoja na kujikuta wakipoteza mwelekeo upande mwingine. Inahitajika kuwa na kikosi kipana ili kumudu kushiriki mashindano tofauti kwa wakati mmoja, mfano ligi ya ndani, Kombe la FA na Ligi ya Mabingwa.

Msimu wa 2018/19, Simba walifanikiwa katika hilo wakiwa chini ya Patrick Aussems kufanya vizuri kimataifa huku pia wakitetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara licha ya kuwa walishindwa kufanya vizuri katika Kombe la FA.

 

MAANDALIZI

Julai, mwaka jana, Simba walienda Afrika Kusini kufanya maandalizi ya msimu huu ambapo walikuwa wakishiriki pia michuano ya kimataifa kutokana na kutwaa kwao ubingwa wa ligi msimu wa 2018/19. Yalikuwa ni maandalizi ya wiki tatu. Muda wa maandalizi ulikuwa mfupi kwao maana waliondolewa katika raundi ya awali licha ya kuwa msimu wa nyuma yake

walitinga hatua ya makundi. Agosti 10, 2019, Simba walitoka suluhu ugenini katika mchezo wa kwanza wa kuwania kuingia makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya UD Songo, wakiwa jijini Dar es Salaam, Agosti 25 wakalazimisha sare ya bao 1-1 na kutupwa nje kwa kanuni ya bao la ugenini. UD Songo kutoka Msumbiji timu aliyokuwa akiichezea Misquissone ilikuwa tayari kwa mashindano kwa sababu ligi yao ilikuwa ikiendelea tofauti na Tanzania ambapo Simba walitoka moja kwa moja katika maandalizi na kucheza mchezo huo, hivyo ni muhimu kwa viongozi kuwa na mikakati ya kufanya maandalizi ya kutosha ili timu iwe tayari.

 

MECHI ZA USHINDANI

Mbali na maandalizi ya kawaida kwa maana ya kuwaweka wachezaji tayari na mashindano ya kimataifa, Simba wanatakiwa kupata michezo kadhaa ya ushindani ambayo itawajenga kumudu kukabiliana na mpinzani ambaye watapangwa naye katika hatua ya awali.

Katika michezo ya kujiweka sawa na mashindano, Simba inatakiwa kupata timu zenye ubora wa juu ili kupata mazoezi ya kutosha vinginevyo inaweza kuwa vigumu kufanya vizuri katika mashindano hayo.

 

MBINU

Hili ni eneo ambalo moja kwa moja linamgusa Kocha Sven Vandenbroeck na benchi la ufundi. Unaweza kuwa mkali wa mbinu katika michezo ya Ligi Kuu, lakini mambo yakawa tofauti katika michezo ya mtoano kama Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kawaida katika ligi ya ndani ukipoteza mchezo mmoja au miwili unaweza kujipanga tena kuhakikisha unafanya vizuri katika michezo ijayo, lakini katika Ligi ya Mabingwa ukipoteza hatua moja unaweza kujikuta ukitupwa nje.

Hivyo Vandenbroeck na benchi la ufundi wanapaswa kujipanga kutumia mbinu ambazo zitawasaidia kufanya vizuri katika michuano hiyo kulingana na kikosi chao.

 

MOTISHA

Miongoni mwa mambo ambayo yamekuwa yakimbeba Kocha José Mourinho anayeinoa Tottenham Hotspur kwa sasa kupata mafanikio ni pamoja na uwezo wa kuhamasisha wachezaji kucheza kwa kujituma. Inaelezwa kuwa msimu wa 2009/10 alikuwa akikaa na mchezaji mmojammoja wakati akiifundisha Inter Milan na kuwajaza upepo ndio maana walitwaa Ligi ya Mabingwa Ulaya. Viongozi wa Simba wanapaswa kuwa na mipango ya namna nzuri zaidi ya kuwapa motisha wachezaji ili kucheza kwa kujituma kama Mourinho na Inter Milan yake.

 

FITNA

Kila kukicha kumekuwa kukiibuka fitna mbalimbali katika soka. Timu moja hufanya ili kuwapunguza nguvu wapinzani wao. Hili sio jambo geni kwa Simba na Yanga ambazo zimekuwa zikishiriki mara kwa mara katika michuano ya kimataifa, hivyo ni vyema Simba ikajipanga juu ya namna ya kukabiliana nazo japo sio kitu cha kukiweka akilini sana kuliko usajili na maandalizi.

 

MSIKIE KOCHA

Kuhusu mikakati yao katika michuano ya kimataifa msimu ujao, Kocha wa Simba, Vandenbroeck alisema: “Mipango yetu kwa sasa ni kumaliza vizuri msimu kwa kutwaa mataji mawili kama itawezekana, baada ya hapo ndipo tutaanza kufanyia kazi mipango iliyopo ya kufanya vizuri katika michuano hiyo.” Michuano ya kimataifa msimu huu ilipangwa kuanza Agosti.