Mbinu za Amunike zaibeba Taifa Stars

Muktasari:

Timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ imewapa furaha mashabiki wa soka nchini, baada ya kuichapa Cape Verde mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Taifa Stars ilipata mabao kupitia kwa washambuliaji wawili wanaocheza soka ya kulipwa nje, Mbwana Samatta na Simon Msuva.

Dar es Salaam. Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jana ulipambwa na nderemo za maelfu ya  mashabiki wa soka waliojitokeza kuishangilia timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ ilipovaana na Cape Verde.

Mabadiliko ya kikosi yaliyofanywa na Kocha Mnigeria Emmanuel Amunike, yalipeleka furaha kwa mashabiki waliokwenda uwanjani kuiunga mkono Taifa Stars.

Licha ya kulala mabao 3-0, katika mchezo wa kwanza uliochezwa siku tano zilizopita mjini Praia, maelfu ya mashabiki hawakukata tamaa kwenda kuipa nguvu timu hiyo.

Mbinu ya Amunike aliyefanya mabadiliko katika kikosi cha jana kulinganisha na kile kilichocheza Praia, ilizaa matunda baada ya Stars kuonyesha kandanda maridadi.

Stars ikicheza kwa kujiamini na kufuata maelekezo ya Amunike, iliwapa raha Watanzania baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Licha ya nahodha Mbwana Samatta kukosa mkwaju wa penalti dakika ya 22 haikuwakatisha tamaa wachezaji wa Stars ambao walicheza kwa ufundi mchezo.

Katika mchezo wa jana, Amunike aliimarisha safu ya ulinzi na kujaza viungo katikati na kuwaacha mbele washambuliaji wawili, Samatta na Simon Msuva.

Amunike aliwaanzisha mchezaji kiraka aliyeongezwa, Erasto Nyoni, Himid Mao, Mudathiri Yahya. Pia upande wa kushoto aliwapanga Gadiel Michael na Abdi Banda ambao wana asili ya ulinzi.

Wakati Gadiel akitokea pembeni kusukuma mbele mashambulizi, Banda alikuwa na kazi moja ya kulinda katika eneo la beki wa kushoto.

Mabadiliko mengine aliyofanya Amunike ni kumpanga beki kisiki Kelvin Yondani ambaye hakucheza mchezo wa awali, kucheza pacha na Aggey Morris na upande wa kulia alicheza Shomari Kapombe.

Yonda aliyecheza badala ya David Mwantika, alicheza kwa kiwango bora na uzoefu wake wa kupanga mabeki wenzake ulikuwa na manufaa.

Katika mchezo wa awali mjini Praia, Kapombe aliingia kujaza nafasi ya Hassani Kessy.

Mbinu ya Amunike ilionekana kuwa na manufaa kwa Stars ambayo ilicheza kufa au kupona kuhakikisha inapata ushindi ili kujiweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa Kundi L.

Awali, Samatta, alikosa penalti dakika ya 22 baada ya shuti lake kugonga mwamba wa juu kabla ya kuokolewa na mabeki wa Cape Verde.

Penalti hiyo ilitokana na Msuva kuangushwa ndani ya eneo la hatari na mwamuzi Souleiman Djama aliamuru penalti hiyo.

Hiyo ilikuwa penalti ya pili Samatta katika kikosi cha Stars, awali alikosa kwenye mechi iliyoisha kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Lesotho, jijini Dar es Salaam.

Samatta anayecheza soka ya kulipwa katika klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji alisawazisha makosa kwa kufanya kazi ya ziada ya kuwatoka mabeki watatu wa Cape Verde na kumimina krosi iliyojazwa wavuni kiufundi na Msuva kwa mguu wa kushoto dakika ya 28.

Stars ilipata bao la pili dakika ya 57 lililongwa kwa shuti kali na Samatta aliyetumia juhudi binafsi kuweka mpira wavuni.

Mshambuliaji huyo aliwapangua mabeki kadhaa wa Cape Verde kabla ya kutengewa mpira mzuri na Mudathir ambapo alifumua shuti lililomshinda kipa Graca Theiry.

Itakumbukwa Stars iliwahi kucheza na Cape Verde kwenye uwanja huo mwaka 2008 ambapo ilishinda mabao 3-1 yaliyofungwa na Jerry Tegete, Athumani Idd ‘Chuji’ na Mrisho Ngassa.

Stars mechi ijayo itakuwa ugenini kuikabili Lesotho Novemba 16, 2018 kabla ya kuhitimisha michezo ya makundi dhidi ya Uganda Machi 22, 2019.

Uganda inaongoza kwa kuwa na pointi saba ikifuatiwa na Cape Verde (nne) na Lesotho (mbili).

Stars: Aishi Manula, Shomari Kapombe, Abdi Banda, Kelvin Yondani, Aggrey Morris, Erasto Nyoni, Himid Mao, Mudathir Yahya, Mbwana Samatta, Simon Msuva na Gadiel Michael.

Cape Verde, Graca Theiry, Ameida Tiago, Rodrigues Carlos, Barros Admilson, Tavares Ianique, Fortes Jeffry, Macedo Elvis, Rodrigues Garry, Soares Luis, Semedo Jorge na Gomes Ricardo.