Mbinu, uwezo kuamua bingwa Simba, Namungo

Sunday August 2 2020

 

By Charles Abel

Dar es Salaam. Karata zitakazochangwa na makocha Thiery Hitimana wa Namungo na Sven Vandenbroeck wa Simba, sambamba na uwezo binafsi wa wachezaji vitaamua bingwa wa Kombe la Shirikisho katika fainali itakayochezwa leo Uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga.

Uwezo wa kucheza kitimu ambao Simba na Namungo zimeonyesha katika mashindano hayo na mengine, unaacha kibarua kigumu kwa makocha kila upande kutafakari na kupanga hesabu na mbinu bora zitakazowezesha timu zao kuibuka na ushindi.

Ikiwa inavizia rekodi ya kuwa timu iliyotwaa taji hilo mara nyingi zaidi ambazo zitakuwa ni mbili, Simba inaingia uwanjani ikiwa na kikosi kilichokamilika ambacho kinampa wigo mpana kocha Vandebroeck kuteua wachezaji 11 watakaoanza.

Hapana shaka Simba itaendelea na mfumo wake ambao umeifanya kuwa tishio msimu huu wa 4-2-3-1, lakini inaweza kubadili na kucheza ule wa 4-4-2 au 3-4-3 kulingana na namna ambavyo Namungo itacheza na ufiti wa wachezaji wake, unampa uhakika Vandenbroeck wa kujua yupi ni mchezaji sahihi wa kuanza kulingana na mbinu atakazotumia.

Vendenbroeck alisema jana kuwa wachezaji wake wote waliosafiri na timu hiyo kwenda Sumbawanga kila mmoja yuko fiti na ana utayari wa kucheza.

“Wachezaji wote wako fiti na yeyote naweza kumtumia katika mchezo wa kesho (leo). Ni mchezo ambao tunahitaji kushinda, hivyo tutatumia wachezaji wetu wote bora ili kuhakikisha tunashinda. Wachezaji wote wapo tayari kwa mchezo,” alisema kocha huyo na kuongeza:

Advertisement

“Tumekuja hapa kucheza fainali na kushinda ubingwa.”

Silaha kubwa kwa Simba katika mchezo huo ni safu yake ya kiungo ambayo imekuwa chachu ya kuzalisha mabao ikiongozwa na Cletous Chamaa ambaye pia ndani ya timu hiyo ndiye kinara wa upachikaji mabao kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho akiwa amefunga matatu, lakini kwenye Ligi Kuu amepiga pasi za mwisho 10.

Kwa upande wa Namungo, kocha Hitimana Thiery upo uwezekano mkubwa akaendelea na mfumo wa 4-4-2 ambao amekuwa akipendelea kuutumia, silaha yake kubwa ikiwa ni mawinga Hashim Manyanya, Abeid Athuma au George Makang’a ambao ndio wamekuwa chachu kutengeneza mashambulizi ya timu hiyo.

Mbali na hao, nyota wengine ambao Hitimana anawategemea waamue mchezo huo ni kiungo Lucas Kikoti na washambuliaji Reliants Lusajo na Blaise Bigirimana, ingawa kulikuwa na taarifa kuwa Lusajo ni majeruhi.

Licha ya ubora wa Simba, Namungo inaingia uwanjani ikitambia nidhamu ya kimbinu ambayo kikosi hicho kinayo na ndio imekuwa chachu kwao kuzipa wakati mgumu timu pinzani hasa zile kubwa za Simba, Azam na Yanga. Pengine hilo ndilo limempa nguvu kocha Hitimana ambaye ametoa tahadhari kwa Simba kuwa wasitegemee urahisi katika mechi hiyo ya fainali.

“Simba ni timu nzuri, lakini hii ni fursa kwa wachezaji wa Namungo kuwa sehemu ya historia kwa kutwaa ubingwa,” alisema Hitimana.

“Jambo la muhimu ni kufanyia kazi kile tulichoelekezana lakini kwa maana ya maandalizi, tupo vizuri na tuko tayari kwa mchezo.”

Mchezo huo utachezeshwa na waamuzi sita ambapo refa wa kati atakuwa Abubakar Mturo, akisaidiwa na washika vibendera Abdallah Mwinyimkuu na Ahamed Arajiga wakati mwamuzi wa akiba akiwa ni Ramadhan Kayoko.

Pia kutakuwa na marefa wawili wa nyuma ya magoli ambao ni Abdulaziz Ally na Hamdan Said.

Timu zote zinaingia zikiwa na rekodi nzuri katika mashindano hayo ambapo Namungo FC imeibuka na ushindi wa ndani ya dakika 90 katika mechi zake zote tano ikifunga mabao manane na kuruhusu mawili, wakati Simba imepachika mabao 14 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara matatu. Hii itakuwa ni mara ya nne kwa timu hizo kukutana ambapo katika awamu tatu zilizopita, Simba imeibuka na ushindi mara moja huku nyingine mbili zikitoka sare.Mara ya kwanza kwa timu hizo kukutana ilikuwa Agosti 18, 2018 pale zilipotoka sare tasa katika mchezo wa kirafiki, lakini zikaja kukutana tena Januari 29, mwaka huu ambapo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 3-2.

Mara ya mwisho kukutana ilikuwa katika mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu msimu huu, uliochezwa Julai 8.

Manahodha wanasemaje?

Nahodha wa Simba, John Bocco alisema wamejipanga kushinda mchezo huo kutokana na maandalizi waliyoyapata..

Naye Hamis Fakhi wa Namungo alisema wanaiheshimu Simba kutokana na ubora wa kikosi chao, lakini lolote linaweza kutokea.

Timu hizo zimetinga fainali baada ya Namungo kuifunga bao 1-0 Sahare All Stars ya mkoani Tanga mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani, huku Simba ikiichakaza Yanga kwa mabao 4-1 katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Taifa (sasa Mkapa) jijini Dar es Salam. (Nyongeza na Mussa Mwangoka)

Advertisement